Thursday , 18 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Samia: Chanzo uhaba maji ni uhujumu wa makusudi
Habari za Siasa

Rais Samia: Chanzo uhaba maji ni uhujumu wa makusudi

Rais Samia Suluhu Hassan
Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema mojawapo ya chanzo cha uhaba wa maji jijini Dar es Salaam ni watu kujenga blocks ‘vizuizi’ kwenye mto Ruvu hali inayoashiria uhujumu wa masukudi kuzuia maji kwenda kutengenezwa na kufanywa kuwa maji safi na salama kwenda kwa wananchi.

Pia amesema katika mchakamchaka waliouendesha kuangalia chanzo cha uhaba wa maji katika mto Ruvu, wamebaini watu wamechepusha maji ili yaende kwenye kilimo na matumizi mengine. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo tarehe 18 Novemba, 2021 wakati akihutubia wananchi katika maadhimisho ya miaka 50 ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando jijini Mwanza.

Aidha, ameagiza wakuu wa mikoa yote, kamati za ulinzi mikoa na wilaya, kuhakikisha wanaweka ulinzi kwenye vyanzo vikuu vya maji na wale wanaochepusha maji wasisite kuchukuliwa hatua za kisheria.

Amesema uhaba wa maji unaopelekea mgawo wa maji na upungufu wa umeme umesababishwa na ubishi na ukaidi wa wanadamu, lakini pili ni kudra za Mwenyezi Mungu.

Pia bado kuna watu wanalima karibu na vyanzo vya maji na haya yote mawili yanapelekea vyanzo vya maji kupungua na hayaendi kule yanakotakiwa yaende.

Akitolea mfano jiji la Dar es Salaam linalotumia mto Ruvu juu na chini ni kwamba kima cha maji kinachochukuliwa kwa kawaida kwa siku katika mto Ruvu chini kimepungua kwa nusu nzima na kufanya mchakato kupeleka maji kwa wananchi kupungua kwa kiasi kikubwa.

“Ndio maana Dar es Salaam kumekuwa na mgawo mkubwa wa maji. Tulipoendesha mchakamchaka, kuangalia kwanini hebu tukatizame kwenye mto kule tumekuta watu wamejenga blocks na kuchepusha maji yaende kwenye kilimo na matumizi mengine.

“Tumekuta magogo na madude gani yamewekwa kuzui maji yasiende kwenye mto. Hii kuna maana mbili, moja kutumika maji kwenye kilimo lakini pili ni uhujumu wa masukudi kuzuia maji kwenda kutengenezwa na kufanywa kuwa maji safi na kwenda kwa wananchi,” amesema Rais Samia.

Pia sababu nyingine ni wanadamu kuingiza mifugo kwenye vyanzo vya maji na taarifa zilizopo ni kwamba kwenye bonde la Mto Ruvu na Ruaha kuna mifugo mingi.

“Wakiingiza mifugo mingi wanaharibu ikolojia na mfumo wa chemchem za maji zilizopo na maji yanakatika mwisho mifugo hawatapata wala wanadamu.

“Vilevile mabadiliko ya tabia nchi ambayo nusu tunasababisha sisi wenyewe kwa kukata miti na kuingiza mifugo kwenye vyanzo vya maji,” amesema.

Aidha, kwa kuwa kudra ya Mungu pia inaweza kuwa sababu, Rais Samia amewaomba viongozi wa dini kuomba dua, Mungu alete mvua zenye Baraka na neema.

“Lakini kutamka tu nasiki gruuu, Mungu ameanza kutusikiliza lakini hii ni kwa eneo moja hapa tulipo huko mengine bado kukavu bado dua zinahitaji Mungu atushushie mvua zenye neema na baraka kwetu,” amesema.

Baada ya kumaliza hotuba yake, baadhi ya viongozi wa dini, Mufti na Sheikh mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir Bin Ally Mbwana, Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Dar es Salaam, Anthony Lusekelo maarufu ‘Mzee wa Upako’ na Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki, Baba Askofu Dk. Flavian Kasalla waliomba dua kisha mvua kidogo kunyesha katika eneo hilo.

3 Comments

  • Duh!
    Nasubiri kalamu ya Mama ichape kazi na kuanza kutumbua.
    Nasubiri huyo mchina ashitakiwe kwa uhujumu uchumi.
    Nasubiri Tanesco walete hasara waliyopata.
    Nasubiri wakazi wote waliokatiwa umeme na kuharibikiwa vyakula na kusafa kwenye joto wafungue kesi ya madai.
    Nasubiri sheria mpya ya maji inayokataza kuvuta maji yaendayo kwenye mitambo ya umeme…hakuna sheria?
    Kazi ianze. Mawaziri wa Maji, Nishati, Uwekezaji na Kilimo wawajibishwe!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za Siasa

CCM yamkana mwenyekiti UVCCM aliyetaka wapinzani wapotezwe

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimejitenga na kauli ya mwenyekiti...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia kutunukiwa udaktari wa heshima Uturuki

Spread the loveBaraza la Chuo Kikuu cha Ankara, ambacho ni cha pili...

error: Content is protected !!