RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa kipande cha tano cha Reli ya Kisasa (SGR), kutoka Mwanza hadi Isaka. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).
Hafla hiyo imefanyika leo Jumatatu, tarehe 14 Juni 2021, katika Kata ya Fera, Wilaya ya Misungwi, jijini Mwanza.
Kiongozi huyo wa Tanzania, ametaja faida tano ambazo Watanzania watazipata wakati wa ujenzi wake na baada ya kuanza kufanya kazi rasmi 2024.
Faida ya kwanza ni, upatikanaji ajira zaidi ya 11,000, wakati ya pili ni kupunguza muda wa usafiri kutoka saa 11, kwa usafiri wa basi hadi kufikia saa nane, kwa usafiri wa treni, kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
Rais Samia amesema faida ya tatu, ni kupungua kwa gharama za usafirishaji mizigo kwa asilimia 40, na kupunguza gharama za bidhaa. Faida ya nne ni kuongeza mapato ya Serikali pindi itakapoanza kufanya kazi.
“Reli hii itasaidia kuchochea shughuli za kiuchumi hasa za uzalishaji, hususan bidhaa za kilimo, uvuvi, viwanda na utalii. Kutakuwa na mabehewa maalumu ya nyama na samaki,” amesema Rais Samia.
Rais Samia ametaja faida ya tano ni reli hiyo kulinda barabara, kwani itasafirisha mizigo mingi, sababu ina uwezo wa kusafirisha mizigo tani 17 hadi 25 milioni, kwa wakati mmoja.
“Itasaidia kulinda barabara zetu, kama mnavyofahamu mizigo mingi inasafirishwa kwa magari na kusababisha kuharibika na hii sababu madereva hawazingatii ukubwa wa mizigo. Itakata takribani maroli 200 kwa wakati mmoja,” amesema Rais Samia.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, amesema ujenzi wa reli hiyo unaogharimu Dola za Marekani 1.326 bilioni (Sh. 3.0617 trilioni, ) unafanywa kwa muda wa miaka mitatu, kuaanzia tarehe 15 Mei 2021 hadi tarehe 16 Aprili 2024.
Kadogosa amesema kipande hicho cha tano cha SGR, kinajengwa kwa urefu wa kilomita 341, ambapo reli hiyo ina uwezo wa kubeba mizigo tani 17 hadi 25 milioni.
“Serikali ya Awamu ya Sita ilitoa Sh. 376.34 bilioni, kumlipa mkandarasi kama sehemu ya malipo ya awali kwa mujibu wa maktaba,” amesema Kadogosa.
Amesema reli hiyo itakuwa na vituo tisa, ikwiemo kituo kikubwa cha mizigo kitakachojengwa Fera mkoani Mwanza.
Kadogosa amesema, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), nayo pia itajenga bandari kavu katika maeneo hayo, kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi jijini humo na katika nchi jirani.
Ujenzi wa reli huo umetanguliwa na vipande vingine viwili, cha kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, chenye urefu wa kilomita 300 na Morogoro hadi Makutupora mkoani Singida, chenye urefu wa kilomita 422, ambavyo vyote vinagharimu Sh. 7.102 trilioni.
Leave a comment