SAMIA Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania amewaomba wananchi kumuunga mkono katika harakati zake kufufua za uchumi. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Pia amewataka wananchi na wanasiasa kuwa na subira kuhusu mchakato ya Katiba Mpya na mikutano ya siasa ya hadhara.
Kuhusu mikutano ya hadhara, Rais Samia amesema “kwa sasa tumeruhusu mikutano ya ndani ya siasa, wabunge kwenye maeneo yao, lakini siyo mbunge atoke eneo lake aende kwingine, lakini ile ya hadhara tujipe muda.”
Akigusia Katiba Mpya amesema “sisemi Katiba si ya maana hapana nipeni muda kwanza tujijenge kiuchumi.”
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, tarehe 28 Juni 2021, Ikulu ya Dar es Salaam wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari, kuhusu siku 100 za utawala wake.

Kiongozi huyo wa nchi aliingia madarakani tarehe 19 Machi 2021, baada ya kifo cha mtangulizi wake, John Pombe Magufuli, kilichotokea 17 Machi 2021 katika Hospitali ya Mzena, Dar es salaam.
“Siku 100 za uongozi wako, Rais tumeona unasimamia haki, uhuru, demokrasia na utawala bora, kumekuwa na swali linaulizwaulizwa lakini hatujapata kauli yako, kuwa Rais anasema nini,” ameuliza Steven Chuwa, mhariri wa ITV na Redio One.
Pia, Mwakilishi wa Idhaa ya Ujerumani (DW), Hawa Bihoga ameuliza “kulikuwa na tamko la marufuku ya mikutano ya kisiasa, lakini sasa umetimiza miaka 100 madarakani, ni lini sasa utatoa tamko ili mikutano iwe rasmi na ni lini utakutana na viongozi wa upinzani kama ulivyoahidi utakutana nao?
Akijibu maswali hayo, amesema “kuna mambo mengi tunataka kuyashughulikia, nimesema tunakwenda kuifungua nchi, uchumi umeshuka tunataka kuupandisha.
“Tukifungua nchi na kwenda kuuweka vizuri, wawekezaji waliosajiliwa kipindi kama hiki Machi hadi sasa ni mara mbili ukilinganisha na mwaka jana,” amesema.
Amesema, wawekezaji wanakuja na tunapofungua hivi, lengo ni wawekezaji wajee wakubwa, fedha zizunguke mfukoni, tukusanye mapato, tukusanye kodi nyingi na hilo linataka nchi iwe na amani na utulivu na nchi iwe inakwenda vizuri.
“Sasa katika kufanya hivyo ni jukumu la kila mmoja kufanya hivyo, uchumi ukipanda unapanda wa kila mmoja, kila mmoja atapata ajira tutaacha kulalamika,” amesema
“Niwaomba sana Watanzania, kama mnavyosema nimeanza vizuri, nipeni muda niisimamishe nchi kiuchumi, halafu tutashughulikia mengine kama Katiba na kukutana na vyama vya siasa,” amesema Rais Samia.
Leave a comment