October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia awapa ujumbe wafanyabiashara Tanzania, Marekani

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema, anatamani kuona biashara kati ya nchi yake na Marekani inaongezeka kwani kwa sasa ni ndogo ikilinganishwa na fursa zilizopo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Amesema hayo jana Jumatano, tarehe 22 Septemba 2021, aliposhiriki mkutano wa pamoja kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na Marekani.

Ametumia fursa hiyo kuhimiza kuimarishwa kwa biashara kati ya mataifa hayo mawili ili kuwa na faida kwa pande zote.

Rais Samia amewaeleza wafanyabiashara hao kwa sasa biashara zinazofanyika kati ya Tanzania na Marekani ni ndogo ikilinganishwa na fursa zilizopo.

Amesema kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2019, Tanzania iliagiza bidhaa zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 241 na kuuza bidhaa zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 46.

Kwa upande mwingine, Marekani imewekeza Tanzania Dola za Kimarekani bilioni 5.55 na kuajiri watu 44,118 wakati Tanzania imewekeza kiasi cha Dola za Kimarekani milioni moja tu ambacho ni kiasi kidogo ikilinganishwa na ukubwa wa uchumi wa Marekani duniani na fursa zilizopo Tanzania.

Rais Samia amewaeleza wafanyabishara hao angependa kuona biashara inaongezeka kwa kuwa Tanzania ni mwanachama katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na pia Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambazo zinatoa fursa za wawekezaji na wafanyabishara wa Marekani kwa soko la watu milioni 450, hivyo kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji.

Aidha, Rais Samia pia amewaeleza wafanyabiashara hao kuwa Tanzania imesaini mkataba wa Biashara Huru Barani Afrika (AfCFTA) ambao umelegeza masharti ya biashara na kuunganisha soko la watu bilioni 1.3.

Taarifa ya kikao hicho kilichofanyikia Marekani, imetolewa na Jaffar Haniu, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu.

error: Content is protected !!