Friday , 19 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Rais Samia awapa makavu wanaharakati “kwangu mimi hakuna kupambana”
Habari MchanganyikoTangulizi

Rais Samia awapa makavu wanaharakati “kwangu mimi hakuna kupambana”

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewataka watetezi wa haki za binadamu waache harakati zenye lengo la kupambana na Serikali bali wafanye harakati zinazoibua masuala chanya yenye kuwasaidia wananchi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 10 ya Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), leo Ijumaa, jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema katika serikali yake hakuna mapambano bali kuna sera za upatanisho, maridhiano na kuwaunganisha Watanzania pamoja.

“Uanaharakati unaweza kuwa vyote, siwakatazi kuwa wanaharakati mnaweza kuwa chanya na au hasi lakini uanaharakati chanya unajenga zaidi. Fanyeni uanaharakati ibueni maovu yanayofanyika. Njooni tukae tuzungumze,” amesema rais Samia.

Mkuu huyo wa nchi, amewataka wanaharakati hao kupeleka malalamiko yao serikalini ili yafanyiwe kazi.

“Hapa wote ni Watanzania hakuna wa kwenda kupambana na Serikali. Unapambana na Serikali kwa jambo gani? Niliwaambia wenzetu wa vyama tunapambana kwa kitu gani wote tunaendesha siasa za Tanzania, lengo letu kuijenga Tanzania,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema “mnajigawa mafungu mnakwenda mnapambana, mnapambana kwa jambo gani? Ndiyo maana tukasema fanyeni harakati za haki za binadamu kulingana na mazingira ya kitanzania, kama mlikuwa wanaharakati wa aluta continua badilikeni wanangu.”

Katika hatua nyingine, Rais Samia ameshangazwa na kitendo cha watetezi wa haki za binadamu, kujikita zaidi katika utetezi wa haki za wanasiasa, badala ya masuala yanayowagusa wananchi ikiwemo wanaopoteza maisha ajalini na wanaojeruhiwa kwa mapanga na vijana wanaofanya uhalifu wa kutumia silaha maarufu kama Panya Road.

Wakati huo huo, Rais Samia alizitaka asasi za kiraia na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, kutoa elimu ya uraia kwa wananchi hususan katiba ya nchi Ibara ya 29 na 30, ili wajue haki zao pamoja na wajibu wao.

“Ndugu zangu mtetezi mkubwa wa haki za binadamu ni katiba yetu ambayo Serikali ndiyo inaitekeleza, ndiyo sheria mama ambayo ina haki zote za wananchi. Swali langu kwenu hawa wanadamu tunaowatetea wanaijua katiba na nataka niache kazi kwenu katika eneo la elimu kwa umma,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema “Muifanye kazi hiyo kuwaelewesha watu wajue katiba yao sababu wanapodai haki lazima wajue na wajibu wao.Niseme kwamba zile haki zilizobainishwa kwenye Ibara ya 29 na 30 ya katiba ziende zikajulikane kwa wananchi.”

Katika hatua nyingine, Rais Samia amewakosoa watetezi wa haki za binadamu kujikita zaidi katika utetezi wa haki za kisiasa na kusahau haki za makundi mengine.

“Nilikuwa najiuliza utetezi wa haki kwa muda mrefu tulikuwa tumejielekeza kwenye kutetea haki lakini hata nyie wana mtandao mmejielekeza zaidi kwenye haki za kisiasa kuliko haki nyingine, nilikuwa nasema kuna tatizo kubwa la ubakaji si Zanzibar hata huku vitoto vinabakwa lakini sauti haijaja juu. Mmekuwa mkitetea haki za wanasiasda kuliko haki za watoto,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia ameonesha kusikitishwa na kitendo cha watetezi wa haki za binadamu kushindwa kukemea uharibifu wa maliasili unaofanywa na baadhi ya watu katika Hifadhi ya Ngorongoro, mkoani Arusha.

Onesmo Olengurumwa, Mratibu wa THRDC

“Wakati napitia kwenye maonesha yenu nimeona muna banda la maliasili wanasema wanatetea haki za maliasili, Tanzania tuna migogoro ya malialisi najua mmefanya kazi mnatoa machapisho, ;lakini ye tunapokwenda kwenye kulinda urithi wa dunia uliopo Tanzania, Serikali inatetea kulinda lakini sio mitandao yenu inayowatetea wanaoharibu urithi wa dunia?” amesema Rais Samia na kuongeza:

“Wanaendelea kubaki na kuharibu urithi wa dunia na ni mitandao yenu inayowatetea kwa mrengo wa kusema haki za binadamu lakini kumbe kuna taasisi ya maliasli je mmekaa wenyewe mkazungumza mkaona lipi lina uzito la kuacha watu waendele kuharibu au tulilinde na wengine watendewe haki wapelekwe pahali pazuri.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB Pesa Akaunti yawavutia wakaguzi wa ndani Afrika

Spread the loveUbunifu wa bidhaa bora wa Benki ya NMB pamoja na...

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari Mchanganyiko

Carbon First, Ruangwa wasaini makubaliano ya biashara ya hewa ukaa

Spread the love  KAMPUNI ya Carbon First Tanzania Limited na Halmashauri ya...

error: Content is protected !!