January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia awapa kazi maalumu Prof. Kabudi, Lukuvi

Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Profesa Palamagamba Kabudi na William Lukuvi ambao amewaweka kando katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, anawapa kazi maalumu ikiwamo kumsaidia kulisimamia baraza hilo la mawaziri. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo tarehe 10 Januari, 2022 jijini Dodoma wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua pamoja na mawaziri.

Amesema kaka zake hao aliowaacha kwenye uteuzi wa mawaziri, umri wao ni sawa na umri wake kwani hata mawaziri aliowateua sasa hawafanani na wawili hao hivyo amewavuta kwake ili wamsimamie kuwasimamia mawaziri.

https://www.youtube.com/watch?v=Mtl4MPA1BYU

“Kwa hiyo kuwaacha kwangu kwenye hiyo listi ni kwa sababu hapo wote ni wadowadogo na mnahitaji kusimamiwa vizuri. Kwa hiyo wawili wale watakuja kwangu tuwasimamie nyie vizuri,” amesema.

PROF KABUDI – BABA MIKATABA

Akimzungumzia Prof. Kabudi, Rais Samia amesema kiongozi huyo aliyekuwa waziri wa sheria na katiba, amefanya kazi nzuri ya kusimamia mazungumzo ya serikali na mashiriki.

“Ndio kazi ambayo nataka nimkabidhi sasa kindakindaki, aendelee na kazi hiyo. Ila kazi yake kwa sababu haipo kwenye muundo haitangazwi wala nini lakini atasimamia hiyo kazi.

“Mashirika yote kazi, zote zitakazoingia ubia na serikali Prof. Kabudi ataongoza hiyo timu, kwa hiyo yeye ni baba mikataba, negotiation,” amesema.

… LUKUVI HAGOMBEI USPIKA

Akimzungumzia Wiliam Lukuvi aliyekuwa waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, Rais Samia amesema ana kazi naye ambayo itafahamika baadaye hivyo watu waache kumchafua kwamba atagombea uspika

“Lakini namvuta Ikulu kazi yetu ni kuwasimamia ninyi. Kwa sababu nikiwatizama hapo wote wanakaribia kustaafu bado miaka miwili, wengine mna safari ndefu, mimi na wale wawili tulishastaafu kwa hiyo kazi yetu sasa ni kushika kiboko kuwasimamia nyie na makatibu wakuu.

“Kwa hiyo msikae hapa mnasema… nimeona meseji nyingi eti afadhali Lukuvi katoka!, hajatoka yupo.

“Wengine wameanza kumletea meseji za ajabu wakidhani atagombania uspika hatagombania uspika ana kazi na mimi … kwa hiyo hatakuwa spika wala hatagombania.

“Msianze kumchafua ametumikia taifa hili kwa uadilifu kwa muda mrefu muache aende na mimi tumalize kazi nitakayompangia,” amesema Rais Samia.

Aidha, amesema tarehe 13 Januari, 2022 atakuwa pamoja na Lukuvi na Kabudi kuwafundisha mawaziri hao walioteuliwa.

“Na tarehe itakayopangwa tutakuwa na makatibu wakuu na manaibu tuna mambo tuelewane kwanza alafu mkafanye kazi,” amesema.

Aidha, ameagiza mawaziri wa wizara zilizomegwa waende wakajipange mapema ili kazi ianze mara moja.

error: Content is protected !!