RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa onyo kwa wanasiasa walioanza kujipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 akisema “kila mwenye nia ya 2025 aache mara moja.” Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Ametoa kauli hiyo leo Alhamis tarehe 01 Aprili 2021, Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, mara baada ya kumaliza kumwapisha Balozi Hussein Kattanga, kuwa Katibu Mkuu Kiongozi.
Pia, amewaapisha mawaziri na naibu mawaziri ambao kwa pamoja aliwateua jana Jumatano tarehe 31 Machi 2021.
Akitoa onyo hilo amesema “nafahamu 2025 iko karibu na kawaida yetu sijui Tanzania au kote ulimwenguni, inapoingia kipindi cha pili cha Rais aliyepo, watu kidogo kunakuwa na hili na lile kuelekea mbele, nataka kuwaambia achene.”
“Twendeni tufanye kazi, hili na lile tutajua mbele. Nataka kusema, rekodi yako inakufuata katika maisha yako na kuna wengine wamekosa hizi nafasi kwa rekodi zako na mimi nitakuwa na jicho kubwa sana pamoja na kwamba yamelegea lakini yanaona.”
Katika kusisitiza hilo, Rais Samia amesema “kila mwenye nia ya 2025 aache mara moja.”
Rais Samia aliyeingia madarakani tarehe 19 Machi 2021, baada ya kufariki kwa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, amewatumia salamu makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walioanza kujipanga kwa uchaguzi ujao.
Dk. Magufuli aliyefariki dunia tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam, akiwa madarakani, alikuwa ameitumikia Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano na miezi mitano.
Alikuwa katika muhula wake wa mwisho wa miaka mitano aliouanza tarehe 5 Novemba 2020 baada ya ule wa awali aliouanza tarehe 5 Novemba 2015 kumalizika na katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, alikuwa amekwisha kusema hatogombea.
Kwa kauli ya Rais Samia aliyeapishwa kushika nafasi ya Rais kwa mujibu wa Katiba kuwa Rais akifariki au kushindwa kuendelea na majukumu, makamu wa Rais ataapishwa, haijafahamika kama ana nia ya kugombea urais mwaka 2025.
Mawaziri walioapishwa ni, Ummy Mwalimu kuwa Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi; Mohammed Mchengerwa (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora) na Seleman Jafo (Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira).
Wengine ni, Prof. Palamagamba Kabudi (Katiba na Sheria), Dk. Mwigulu Nchemba (Fedha na Mipango), Dk. Kitila Mkumbo (Viwanda na Biashara), Goefrey Mwambe (Uwekezaji) na Balozi Liberata Mulamula (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki).
Naibu waziri walioapishwa ni, Naibu waziri Ofisi Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, Hamad Hassan Chande, William Tate Olenasha (Uwekezaji), Abdallah Ulega (Mifugo na Uvuvi) na Mwita Waitara (Ujenzi na Uchukuzi).
Pia, Pauline Gekul (Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo), Mwanaidi Ally Hamid (Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto).
Leave a comment