RAIS Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza watu 17 waliofariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea mkoani Tanga, wakiwa njiani kutokea jijini Dar es Salaam, kupeleka maiti mkoani Kilimanjaro. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Mkuu huyo wa nchi ametuma salamu hizo asubuhi ya leo Jumamosi, baada ya ajali hiyo kutokea usiku wa jana tarehe 3 Februari 2023, eneo la Magila Gereza, wilayani Korogwe, Mkoa wa Tanga.
“Nimesikitishwa na vifo vya watu 17 vilivyosababishwa na ajali iliyotokea jana saa 4:30 usiku eneo la Magila Gereza, Wilaya ya Korogwe, Mkoa wa Tanga. Nawapa pole wafiwa na wote walioguswa na vifo hivi. Nawaombea ndugu zetu hawa wapumzike mahali pema na majeruhi wapone haraka,” ameandika Rais Samia katika ukurasa wake wa Twitter.
Nimesikitishwa na vifo vya watu 17 vilivyosababishwa na ajali iliyotokea jana saa 4:30 usiku eneo la Magila Gereza, Wilaya ya Korogwe, Mkoa wa Tanga. Nawapa pole wafiwa na wote walioguswa na vifo hivi. Nawaombea ndugu zetu hawa wapumzike mahali pema na majeruhi wapone haraka.
— Samia Suluhu (@SuluhuSamia) February 4, 2023
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba, akithibitisha ajali hiyo alisema ajali hiyo imehusisha gari aina ya Mitsubishi Fuso iliyogonga gari aina ya Coaster iliyokuwa imebeba mwili wa marehemu na abiria 26, ikitokea Dar es Salaam kwenda Moshi, kwa ajili ya mazishi.
Alisema waliofariki kwenye ajali hiyo ni wanaume tisa, wanawake sita na watoto wawili.
Katika ajali hiyo kulikuwa na majeruhi 10 wa ajali hiyo wamepelkwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, Bombo kwa ajili ya matibabu.
Leave a comment