December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia awafunda mabalozi, awapa mwelekeo mpya

Rais Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi kuangalia vipaumbele vya Taifa ikiwemo kufanya mapitio ya sera ya mambo ya nje na kuioanisha na mabadiliko yaliyotokea duniani hususani ya kiuchumi na kijamii. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Akizungumza leo tarehe 19 Novemba, 2022 Visiwani Zanzibar katika mkutano wa mabalozi hao, Rais Samia amesema sera hiyo ya mambo ya nje imedumu kwa miaka 20 sasa hivyo inapaswa kufanyiwa mapitio ili kuendana na hali iliyopo duniani.

Amewataka mabalozi kutumia kikao hicho kutafakari mabadiliko hayo ambayo ni pamoja na matishio mapya ya usalama na ustawi wa nchi, mabadiliko ya tabianchi, majanga ya afya, uhalifu wa kimataifa na mapinduzi ya nne ya viwanda.

Pia mabadiliko mengine yaliyotokea duniani ni pamoja na kurudi kwa siasa za kuvutana baina ya mafahali wa dunia na kutaka kuziburuza nchi za Afrika katika migogoro yenye masilahi kwao huku athari za migogoro hiyo zikiangukia kwenye bei za nishati, chakula na sarafu duniani.

“Jingine kubadilika kwa mwelekeo wa uchumi wa duniani, ambapo ukuaji mkubwa wa uchumi ikiwemo uzalishaji, uendeshaji, biashara ubunifu na uvumbuzi sasa vimehamia kwenye bara moja la Asia ambalo linazalisha takribani asilimia 40 ya pato la dunia (GDP). Kwa hiyo nasi ni vema kujadili tunaingia vipi ili kufaidika na bara hilo,” amesema.

Aidha, amesema kuonengeza kwa kasi ya utangamano katika bara la Afrika ikiwemo kupanuka kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyoongeza wanachama kutoka watano hadi saba, nalo ni jambo la kujadili ili Tanzania inufaike na utangamano huo.

“Kuna suala la kutekeleza kwa itifaki ya soko huru la Afrika, kuibuka kwa mahitaji mapya ya ndani ikiwemo kukua kwa uchumi wa bluu, kutanuka kwa matumizi ya lugha yetu ya Kiswahili duniani pamoja na suala la ndugu zetu wanaoshi nje, tunatakiwa kuangalia jinsi wanavyochangia nyumbani na masilahi yao kule walipo,” amesema.

Amesema kutokana na mabadiliko hayo makubwa, ni lazima kufanya mapitio ya sera hiyo ya mambo ya nje ili iendane na hali ya sasa.

Amesema Tanzania ina sera mbili kuu; ya kwanza sera ya ndani ambayo hujumuisha sera zote za ndani zenye lengo la kuendeleza na kustawisha Taifa.

Amesema sera hizo za maendeleo ya kiuchumi au kijamii hutengeneza kinachoitwa masilahi ya taifa.

“Hii ndio dhima ninayoiendeleza, ninaangalia mema yaliyopita na kuangalia mema yaliyopo na kupanga maboresho ya kufanya mema tunapokwenda, hiyo ndio spirit ya wote nami naendeleza,” amesema.

Amesema sera ya pili ni sera ya mambo ya nje ambayo hutafsiri sera za ndani kwa mawanda ya mapana ya sera za kimataifa kwa masilahi Taifa.

Amesema sera hiyo inatekelezwa na wadau wengi chini ya uratibu wa wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki.

“Hili ndilo jukumu lenu mabalozi kwenye maeneo yenu ya uwakilishi, kuchukua sera zetu za ndani na kuzioanisha na sera zenu za nje na kupanga vile mtakavyotekeleza kila mtu kwa eneo lake kuleta masilahi nyumbani,” amesema.

Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu aliokaa madarakani ameteua mabalozi 61 kati yao wakiwa ni wale walioongezewa mikataba.

“Kati yao 16 wakiwa ni watumishi wa kada ya nje kutoka ndani ya wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki na katika hao wanawake ni 13 na vijana chini ya umri miaka 45 ni 4.

“Lengo la kuongeza urari wa jinsia katika diplomasia yetu na kuipa uhai mpya, kuzingatia damu mpya na kuandaa kizazi kijacho cha wanadiplomasia mahiri kama wale tuliowahi kuwa nao huko nyuma ambao wengi wao sasa wamestaafu,” amesema.

error: Content is protected !!