August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia aunda Kamati kufumua vyombo vya haki jinai

Rais Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan ameunda Kamati ya watu 12 na sekretarieti ya watu watano kwaajili ya kuchunguza na kumshauri muundo mzuri wa vyombo vya haki jinai. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Rais Samia amebainisha hay oleo Jumatano tarehe 20 Julai, 2022, mara baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali akiwemo Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi, Camilius Wambura.

Mkuu huyo wa nchi amesema Kamati hiyo itaongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu, Othman Chande akisaidiwa na Makamu Mwenyekiti Ombeni Sefue na kwamba wajumbe wengine watafahamika baadae.

“Nimeunda kamati kunishauri namna ya kuleta mabadiliko ya utendaji kazi wenye matokeo bora kwenye vyombo vyetu vya haki jinai, kwahiyo tutaanza na polisi tukimaliza wataleta mapendekezo, tunakwenda majeshi mengine yote,” amesema Rais Samia.

“Serikali sasa tunakuja na jicho jingine ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama Tanzania, tunakwenda kusimamia haki, hii kamati yangu itaniletea mrejesho kila jeshi linapomaliza kuchunguzwa na kufanyiwa maboresho, tutakuja na miundo inayofaa sasa hivi ili kujenga majeshi imara na bora kutumikia watanzania,” amesisitiza.

Rais Samia amempongeza IGP Wambura kwa kazi ambazo amefanya ndani ya polisi muda wote na kwa kuteuliwa katika nafasi hiyo, “nachotegemea ni kuona mabadiliko, ufanisi, usalama wa raia na mali zao unaimarika ndani ya Jeshi la Polisi.”

Samia amesema katika “dhana” ya utawala bora suala la haki kwa wananchi “linapaswa kupewa kipaumbele kikubwa kwa maana hiyo nimeamua kufanya mabadiliko ya mfumo kwenye taasisi zetu za haki jamii.”

Amezitaja taasisi hizo kuwa ni Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mashitaka, TAKUKURU, Jeshi la Magereza na Mamlaka ya kupambana na dawa za kulevya, “zote lazima tufanyie marekebisho kwa kuangalia miundo ikoje, je inasaidia leo inaleta ufanisi leo, inakwenda na yaliyopo duniani?”

Samia amesema katika mabadiliko hayo wataangalia mifumo ya ajira, mafunzo, maadili na nidhamu sambamba na kuangalia mifumo ya utendaji kazi.

“Lazima tuangalie tunakwendaje, tunakwenda kama kanuni zinavyotutaka, kama sheria zinavyosema, au tumezoeana mno kiasi ambacho tunafanya tu na hatuwezi kuchukuliana hatua yeyote,” amesema.

Ameongeza kuwa licha ya kuwa kuna taasisi zinazojitahidi kuchukua hatua lakini amekuwa akipokea lawama kutoka kwa wanaochukuliwa hatua.

“Ukiuliza kafanya nini kafukuzwa, unaletewa mambo unasema tena ulichelewa kumfukuza.”
Mbali na hayo amesema wanakwenda kuangalia mifumo ya upandishaji vyeo na kuhakikisha wanaopandishwa wanakuwa na sifa.

Pia amesema upatikanaji wa watendaji kazi utaangaliwa kwa kuhakikisha wanaochaguliwa kujiunga na vyombo hivyo wanakuwa na sifa pamoja na kufaulu mafunzo ipasavyo.

error: Content is protected !!