May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia atumbua vigogo watatu, avunja bodi

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa viongozi watatu na kuivunja Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Tanzania. Anaripoti Nasra Bakari, DMC … (endelea).

Taarifa iliyotolewa leo tarehe 03 Mei, 2021 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga imeeleza uteuzi wa viongozi hao umetenguliwa kuanzia tarehe 30 Aprili, 2021.

Kwanza, Rais Samia ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) Profesa Tadeo Andrew Satta, ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).

Sambamba na hatua hiyo, Rais Samia pia ametengua uteuzi wa wajumbe sita wa bodi ya TASAC.

Profesa Satta, aliteuliwa na Hayati Rais John Magufuli, kushika wadhifa huo, tarehe 23 Aprili 2019 pamoja na wajumbe wake sita.

Wajumbe hao walioteuliwa ambao nao wametenguliwa ni; Evelyne Makala, Renatus Mkinga, Japhet Massele, Daniel Mchome, Mussa Mandia na Bernard Asubisye.

Hivi karibuni, Rais Samia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Emmanuel Ndomba na kumteua Kaimu Abdi Mkeyenge.
Rais Samia, alimuagiza Mkeyenge kwenye kuangalia shirika hilo kwani limekuwa likiendesha vikao vya bodi na kulipana mamilioni ya fedha.

Pili, Rais Samia ametengua uteuzi wa Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Hassan Mwang’ombe.

Tatu, Rais Samia ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Tanzania, Dk. Harun Kondo.

Sambamba na hatua hiyo, Rais Samia pia amevunja Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Tanzania.

Uteuzi wa viongozi watakaoshika nyadhifa hizo utafanywa baadaye.

error: Content is protected !!