May 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia atuma salamu kwa wanaombeza

Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewataka wale wote wenye shaka ya uongozi wake kutokana na jinsia yake ya mwanamke, kukaa mguu sawa. Anaripoti Regina Mkonde, Dodoma … (endelea).

Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, tarehe 22 Machi 2021, katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, wakati akihutubia maelfu ya waombolezaji, aliojitokeza kuuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli.

Dk. Magufuli, alifariki dunia 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa mfumo wa umeme wa moyo.

Mara baada ya kufariki, Mama Samia, aliyekuwa makamu wa Rais, kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, akaapishwa kuwa Rais wa Tanzania.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Samia amesema “kupitia Rais Magufuli, Tanzania ilipata mwanamke wa kwanza kuwa makamu wa Rais na sasa Tanzania imepata mwanamke wa kwanza Rais. Kumbe mwanamke anaweza akipewa fursa sawa.”

“Na wale wenye mashaka kuwa mwanamke huyu anaweza kuwa Rais, nataka kuwahakikishia huyu aliyesimama hapa (yeye Mama Samia) ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye maumbile yake ni mwanamke,” amesema Rais Samia.

Mara baada ya kauli hiyo, shangwe zillipuka na kusikika wakisema ‘CCM, CCM, CCM.”

Mama Samia amesema, kifo cha Rais Magufuli ni pigo kubwa kwani “mbele yangu na mbele yenu, mnaona mwili wa mpendwa wetu Dk. Magufuli ukiwa umelala, lakini leo nimekaa katika kiti ambacho alikuwa akikaa yeye. Kwa kweli kifo ni fumbo kubwa sana.”

“Naomba kuwahakikishia, hakuna jambo litakalohalibika, nchi yetu iko salama na mimi na mwenzangu Dk. Hussein Ali Mwinyi (Rais wa Zanzibar), tutayaendeleza yale aliyoyaanzisha,” amesema

Pia, Rais Samia amewahakikishia nchi mbalimbali kwamba, yuko tayari kufanya nao kazi kama kawaida.

Rais Samia amewaomba Watanzania “kuendelea kuwa na utulivu mkubwa katika kushikamana na kuomboleza ili mpendwa wetu alale salama.”

Pia, amevishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha wananchi wanaoomboleza wanakuwa katika hali ya amani na utulivu na navishukuru sana vyombo vya habari kwa kuwaelimisha vizuri.

error: Content is protected !!