RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, leo Jumatatu tarehe 16 Agosti, 2021 amewasili Lilongwe nchini Malawi kushiriki Mkutano wa 41 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Mkutano huo utaanza kesho Jumanne 17-18 Agosti 2021.
Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kamuzu, Rais Samia amepokelewa na Patricia Kaliati, Waziri wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii wa Malawi.
Katika Mkutano huo wa 41 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC, Jamhuri ya Malawi itathibitishwa kuwa Mwenyekiti wa SADC kwa kipindi cha mwaka mmoja (Agosti 2021 – Agosti 2022).
Aidha, Wakuu hao wa Nchi na Serikali watamthibitisha Katibu Mtendaji mpya wa SADC baada ya Katibu Mtendaji aliyepo Dk. Stergomena Tax kumaliza muda wake baada ya kuhudumu kwa ufanisi nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka nane.
Wakuu hao wa Nchi na Serikali wa SADC pia wanatarajiwa kujadili masuala mbalimbali ya Mtangamano pamoja na kuidhinisha kauli mbiu ya Jumuiya hiyo.
Taarifa ya kuwasili kwa Rais Samia imetolewa na Jaffar Haniu, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
Leave a comment