October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia atua Dodoma, apewa zawadi

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewasili Jijini Dodoma akitokea mkoani Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Rais Samia amewasili jana Jumapili, tarehe 26 Septemba 2021 na kupokelewa na wananchi wa Jiji hilo wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, Mawaziri, Wabunge mbalimbali pamoja na Madiwani.

Amewashukuru wananchi wa Jiji la Dodoma kwa kujitokeza kwa wingi kumpokea na kueleza mbali na kuhudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lakini pia imemuwezesha kukutana na marais wenzake na Wakuu wa Taasisi mbalimbali na kuahidiwa kuwa wapo tayari kufanya kazi na Serikali ya Tanzania katika kuwaletea Wananchi maendeleo.

Aidha, Rais Samia amesema katika kipindi cha miezi sita tangu Serikali ya awamu ya sita kuingia madarakani idadi ya wawekezaji na wafanyabiashara wameongezeka kwa kiwango kikubwa hivyo kuchochea kasi ya maendeleo.

Mara baada ya kuwasili Chamwino, Rais Samia amepokelewa na wakazi wa Wilaya hiyo ambao walimkaribisha rasmi kama mkazi mwenzao na kumpatia zawadi ya Ng’ombe wa maziwa, kumvika mavazi ya kimila na kumkabidhi Ngao na Mkuki kama ishara ya Kinga na Ulinzi wa Nchi.

Rais Samia amewahakikishia wananchi hao atahakikisha anazitatua changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na zile zilizoahidiwa na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano Hayati John Pombe Magufuli.

Aidha, Rais Samia ameahidi wananchi hao kuwa Serikali itaboresha huduma za jamii ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama, madarasa ya wanafunzi pamoja na kuwajengea Soko la biashara.

Rais Samia amewaomba wananchi wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla kuendelea kudumisha amani ili kuiwezesha Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo na kukuza uchumi wa nchi.

Taarifa hiyo, imetolewa na Jaffar Haniu, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

error: Content is protected !!