Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Samia atoboa siri Mama Mkapa alivyomuingiza kwenye siasa
Habari za Siasa

Rais Samia atoboa siri Mama Mkapa alivyomuingiza kwenye siasa

Rais Samia Suluhu Hassan
Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Mwenyekiti wa Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF), Mama Anna Mkapa ndiye aliyemjengea uwezo na kumshika mkono hadi kuingia kwenye siasa mwaka 2000.

Amesema nguvu ya kuingia kwenye siasa ni maneno ya mama Anna Mkapa ambaye alimbeba kwenye gari yake baada ya kuachwa na basi la wafanyakazi wenzio mwaka 1999 alipokuwa ameajiriwa na Mfuko huo wa EOTF. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akisimulia mkasa huo leo tarehe 27 Juni, 2022 jijini Dar es Salaam katika Sherehe za maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Fursa sawa kwa wote, Rais Samia amekiri kuwa EOTF ndio iliyomjengea uwezo kuingia kwenye siasa.

Amesema alijiunga na EOTF mwaka 1997 akiwa mmoja wa wajumbe wa Bodi ya wadhamini tena kijana machachari.

“Nakumbuka siku moja tulienda kutembelea akina Rugimbana kule Chamazi… tulikuwa tunaenda kutembelea kijiji cha vijana. Watu wote waliingia kwenye magari mimi nimezubaa, Mama Mkapa akaniona nimezubaa akaniuliza wewe Mpemba vipi! nikamjibu magari yamenikimbia… akasema hebu ingia humu.

“Unaweza kupata picha kwamba Mama wa Rais anapakia mtu kama mimi ndani ya gari lake. Ndani ya gari lake akaniambia nimekuona toka umekuja, unavyokwenda na unavyofanya wewe ni mwanasiasa mzuri. Uchaguzi unaokuja ungejaribu, akaniambia uliza huko kwenu Pemba uliza utaingia.

“Tukafanya kazi, nikarudi kwa basi na mama akarudi peke yake kwenye gari yake,” amesema.

Amesema Mama Mkapa alimweleza maneno hayo mwaka 1999 ambapo yalimkaa kichwani lakini akawa anajiuliza ataanzia wapi… hata hivyo, akajipa moyo kwa kuwa atajaribu kwa kuwa Mama Mkapa amemueleza anaweza.

“Upande mwingine nilikuwa nakerwa na majibu yanayotoka ndani ya Baraza la wawakilishi kuhusu shida za wananchi, nikasema nadhani mama ameniambia niende, nadhani kule ndio kwenye kazi yangu basi nikajaribu.

“Nilipojaribu nikashikwa mkono vizuri, nikaingia nikawa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na safari ikaanza hapo moja kwa moja waziri, awamu ya pili waziri, awamu ya tatu waziri ofisi ya makamu wa rais, nimegombea tena mgombea mwenza, safari imenifikisha hapa.

“Lakini nguvu ya kuingia ni maneno ya mama Anna Mkapa ambaye alinichukua kwenye gari yake. Nadhani Mungu alinifanya nizubae nikimbiwe ili niingie kwenye hiyo gari nikapate hiyo nguvu. Kwa hiyo nami ni mmoja wa wafaidika walioibuliwa na EOTF,” amesema Rais Samia.

Amesema licha ya kwamba wakati anaingia EOTF ailikuwa nafanya World Food Program huko Zanzibar, anaishukuru taasisi hiyo kwa kumjengea uwezo.

Mama Anna Mkapa

“Nashukuru kujengewa uwezo kufika hapa. Tupo wengi tuliojengewa uwezo, nakumbuka Lazaro Nyalandu, Jacob na vijana wengi tumepita mikono hii.

“Kwa hiyo Mama Mkapa tunakushukuru sana pamoja na kulea wanawake 6000 ambao wanafanyabiashara ndani na nje ya nchi, Mungu akupe uwezo zaidi, akuweke akupe maisha marefu uweze kulea wengine na wengine nasi tuliofaidika nawe tupo nyuma kukusaidia,” amesema.

Aidha, amesema kitendo cha Mama Mkapa kukaa na wanawake kwa miaka 25 hadi lsasa, ameonesha uwezi mkubwa kwa kuwajengea uwezo wa kiuchimi na kimaendeleo, vijana na wanawake.

Amesema kutokana na ukubwa wa nchi, tofauti zake za kimazingira,na kibajeti anatoa wito wa kushirikiana na kukaribisha mashirika binafsi, taasisi za kidini kutoa na kuchangia maendeleo kwa wanaoishi mazingira duni.

“Kazi ya kupiga vita umaskini, ujinga na maradhi lazima iwe shirikishi. Lazima kuinga mkono serikali katika nyanja zote,” amesema.

Aidha, ametoa wito kwa Watanzania kuhamasisha wazazi kutowatelekeza watoto wetu kwani wanapowatelekeza na asipotokea mtu wa kuwaokota na kuwaweka pamoja na kuwaendeleza, huenda Taifa likazalisha panya roads wengi wanaomsumbua Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaa, Amos Makala.

Pamoja na mambo mengine ameahidi kuendelea kushirikiana na mfuko huo na taasisi nyingine kadiri inavyowezekana katika kutafutia ufumbuzi changamoto, ikiwamo michango, watumishi na madawa, na eneo na fedha za kujenga jengo hilo la wanawake.

Amemuagiza Makala kuwatafutia EOTF eneo la ujenzi wa jingo hilo, kisha yeye atahangaika na fedha za kujenga hilo eneo.

1 Comment

  • Duh!
    Samia, kuna watu walisema ni kazi ya Kikwete lakini umetuaminisha sasa!
    Hongera kwa kuwa jasiri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Chadema: Samia aunde tume kuchunguza mauaji mgodi wa Barick

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ameombwa aunde tume huru kwa...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

error: Content is protected !!