May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia atoa utaratibu mpya maiti kutokuzuiwa

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amemuagiza Waziri wa Afya, Dk. Dorothy Gwajima, aandae utaratibu mpya wa malipo ya madeni ya gharama za matibabu, za wagonjwa wanaofariki dunia, ili kuondoa changamoto ya maiti kuzuiwa hospitalini. Anaripoti Nasra Bakari, DMC…(endelea).

Rais Samia ametoa agizo hilo leo Jumanne, tarehe 8 Juni 2021, akizungumza na wanawake wa Mkoa wa Dodoma.

“Hili la kudaiwa wakati mgonjwa amefariki, waziri wekeni mpango mzuri. Ambapo kama mgonjwa amefariki, maiti yake itatolewa. Kweli kidini tunaambiwa mtu asiende kuzikwa mpaka deni liwe limelipwa, lakini si deni la Serikali,” amesema Rais Samia.

Kiongozi huyo wa Tanzania, ameitaka wizara hiyo kuweka utaratibu utakaowezesha ndugu na jamaa wanaofiwa, kulipa madeni ya gharama za matibabu, baada ya kumzika ndugu yao.

“Naomba muweke mpango mzuri na hapa nataka wananchi wanielewe, sio kwamba deni lisilipwe bali kuwekwe mpango mzuri wa kulipa deni bila kuzuia maiti,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia ametoa wito kwa wananchi, kulipa gharama za matibabu wakati mgonjwa anaendelea kupata huduma hiyo, ili kuepuka mrundikano wa madeni, ambao hawataweza kulipa kwa wakati mmoja.

“Na mpango mzuri ni kutoa gharama za matibabu wakati matibabu yanaendelea, bila kusubiri siku ya mwisho mgonjwa amefariki, unamwambia milioni tatu huku ana maiti ya kusafirisha. Ana deni maiti hatoki bila kuilipa. Naomba muweke mpango mzuri kushughulikia hili,” amesema Rais Samia.

error: Content is protected !!