June 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia atoa onyo kwa Ma RC, RAS

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

SAMIA Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania, ametoa onyo kwa wakuu wa mikoa (RC) na makatibu tawala wa mikoa (RAS), kufanya kazi kwa ushirikiano na watakaobainika kwende kinyume atachukua hatua. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Rais Samia, ametoa onyo hilo, leo Jumatano, tarehe 2 Juni 2021, Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma, wakati akiwaapisha makatibu tawala wa mikoa, aliowateua wiki iliyopita.

Amesema, kumekuwa na kawaida ya RC na RAS kutofautiana na wakati mwingine, mkoa wenye Ma RC au RAS wanawake, kuonyeshana umwamba jambo ambalo hatapenda litokee kwani litamfanya asemwe.

Rais Samia amesema, ma RAS kwa sasa ni asilimia 46 wanawake na 54 ni wanaume na amefanya hivyo kwa kutambua, wanawake wanaweza kuongoza.

“Asilimia 46 ya wanawake kwa makatibu tawala wa mikoa, nimefanya hivi nikijua mnauwezo mkubwa wa kufanya kazi. Kazi hii mnaiweza na tunataka kuona mabadiliko ya wanaume walipokuwa wengi na sasa wanawake mnakaribiana na wanaume, hali itakuwaje,” amesema Rais Samia

“Ile mikoa yenye mkuu wa mkoa mwanamke na katibu tawala mwanamke, msianze zile kauli usinibabaishe. Mtanikwaza na mwende mkachape kazi. Isianze ile kauli ya wanawake hawakai pamoja mbona wanaolewa pamoja,” amesema

Kuhusu kudharauliana, Rais Samia amesema, kulijitokeza hali hiyo wakati Anna Mghwira, alipoteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro.

Mghwira, aliyestaafu kwa sasa, aliteuliwa mwaka 2017 na Hayati Rais John Pombe Magufuli, wakati huo akiwa Mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo.

Rais Samia amesema, naye amefanya hivyo kwa kumteua Queen Sendiga kuwa mkuu wa mkoa wa Iringa. Sendiga mpaka sasa ni Naibu Katibu Mkuu Bara wa chama cha ADC.

“Tuna uzoefu tulipomweka Anna Mghwira kule Kilimanjaro, wakuu wa wilaya walimdharau. Qeen umekwenda Iringa, nendani mkafanye kazi sawa kwa sawa, mheshimiane, mjenge ushirikiano na mpendane, sijui huyu si wa kwetu, sijui katoka wapi sitaki kusikia,” amesema

Amewataka makatibu tawala wa mikoa, kwenda kuwashauri vyema wakuu wa mikoa ili kuhakikisha mikoa yao inasonga mbele kimaendeleo na kutatua matatizo ya wananchi.

Katika kusisitiza hilo, Rais Samia amesema “kila niliyemteua kuna mtu nyuma na hujui kuna nani. Sitanii katika hili, nendeni mkafanye kazi.”

“Kila mtumishi apate haki yake, kama amefikia kupanda cheo apande, anastahiki hiki apate, kuna uonevu na uzembe mkubwa huko mikoani,” amesema.

error: Content is protected !!