September 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia atoa milioni 500 ujenzi wa kituo cha afya Narungombe

Rais Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameshirikiana na wananchi kusafisha eneo ambalo litajengwa kituo cha Afya Katika kata ya Narungombe, Ruangwa mkoani Lindi. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Akizungumza na wananchi katika eneo hilo, leo Jumamosi tarehe 4 Septemba 2021,

Majaliwa amesema, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa Sh. 500 milioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho ambacho kitahudumia wakazi wa Vijiji vya Nangurugai, Machang’nja, Chikwale, Chiundu, Liuguru, Itumbi, Nkoma na sehemu ya Chunyu

“Rais wetu Samia Suluhu Hassan ameamua kuimarisha sekta ya afya kwa kuimarisha vituo vyote vya kutolea huduma, kituo hiki litawekwa eneo la kupokea wagonjwa na sehemu ya madaktari hadi watano kusikiliza wagonjwa,” amesema

Amesema “kutakuwa na maabara kubwa, jengo la mama na mtoto ikiwemo chumba cha upasuaji, kutakuwa na eneo la watoto njiti na kutakuwa na jengo kwa ajili ya upasuaji mdogo, wa kati na mkubwa.”

Majaliwa amesema, baada ya kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya kituo hicho, Rais Samia ameahidi kuwa atatoa Sh.250 milioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa ikiwemo vya upasuaji na vipimo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Aidha, Majaliwa amemuagiza Mwenyekiti wa Kijiji Narungombe, Rashidi Omari Chijuni kuunda kamati kwa ajili ya kusimamia ujenzi wa kituo hicho ili kuhakikisha ujenzi wake unakamilika katika muda uliokusudiwa “tuoneshe umakini katika hili, wananchi hawa wote wanahitaji huduma kutoka katika kituo hiki.”

Akizungumza kwa niaba ya Wazee wa Kijiji cha Narungombe, Mzee Selemani amewashukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa kutekeleza ahadi ya ujenzi wa Kituo cha Afya Narungombe.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi wa kijiji hicho wamemshukuru Rais Samia kwa kuamua kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho, kwani kitawapunguzia adha ya kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta huduma za afya.

Awali, Waziri Mkuu alikagua maendeleo ya ujenzi wa Ghala ya kuhifadhia mazao la Chama cha Ushirika cha RUNALI na baadae kukagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa.

error: Content is protected !!