RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa Sh.100 milioni kwa ajili ya ujenzi wa paa la kisasa la kuzuia jua na mvua kwa wahanga 1,800 wa Soko la Kariakoo waliohamishiwa Machinga Complex. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Soko la Kariakoo upande wa juu, liliteketea kwa moto usiku wa Jumamosi tarehe 10 Julai 2021, kuamkia Jumapili. Chanzo cha moto huo bado haujajulikana.
Jumapili ya tarehe 11 Julai 2021, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitembelea soko hilo na kitangaza kulifunga kwa kipindi cha siku saba ili kupisha tume aliyoiunda kuchunguza chanzo cha moto huo ili kubaini nini kimesababisha au nani kasababisha moto huo. Ripoti yake bado haijawekwa wazi.
Leo Jumanne, tarehe 20 Julai 2021, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla akizungumza na wafanyabiashara katika soko la Machinga Complex amesema, amepokea Sh.100 milioni kutoka kwa Rais Samia.
Amesema baada ya jana Jumatatu, kuwatembelea na kuwasikiliza, Rais Samia aliona changamoto hiyo na alipomuuliza kiasi cha fedha kinachohitajika alisema ni Sh.62 milioni za ujenzi wa paa la turubai.
Makalla amesema, kwa kutambua umuhimu wa wafanyabiashara, Rais Samia alitoa Sh.100 milioni ili lijengwe paa la kudumu kwa bati la kisasa.
Kutoka na fedha kupatikana, RC Makalla amewaelekeza Suma JKT ambao ndio wajenzi kuanza ujenzi mara moja ili wafanyabiashara hao wafanye biashara bila kero.

Kuhusu suala la meza, RC Makalla amesema tayari amepatikana mkandarasi atakaejenga meza za kisasa za kuhamishika kuendana na hadhi ya soko.
Aidha, Makalla ameelekeza viongozi wa Jiji la Ilala kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya taka, mifumo ya maji, mifumo ya umeme na wafunge vizima moto ili kukabiliana na majanga ya moto.
Leave a comment