May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia atoa matumaini nyongeza ya mishahara

Spread the love

RAIS Samia Suluhu Hassan ameendelea kutoa matumaini ya nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi nchini baada ya kuwadhibitishia kuwa atapandisha kima cha chini cha mishahara baada ya mahesabu kukamilika. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo tarehe 1 Mei, 2022 kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi duniani yaliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Amesema ulezi wake kwa wafanyakazi unaendelea hususani katika yale aliyoyafanya mwaka jana na mwaka huu ataendelea kuyafanya lakini pamoja na hayo lile jambo lao (nyongeza ya mishahara) lipo.

“Jambo letu lipo si kwa kiwango kilichosemwa na TUCTA kwa sababu mnajua hali ya uchumi wa nchi yetu na uchumi wa duniani, hali si nzuri sana.

“Uchumi wetu ulishuka chini mno, tumejitahidi sana na kwa sababu nilishatoa ahadi mwaka jana kwa hiyo nimeagiza jambo liwepo… mahesabu yanaendelea tutajua lipo kwa kiasi ghani lakini jambo lipo,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amesema tayari serikali imeshaunda bodi za kima cha chini cha mishahara kwa sekta zote za umma na binafsi na tayari zimeanza kufanya tathmini ili kufanya maboresho ya kima cha chini cha mishahara kilichopo sasa.

“Kwenye jambo hili ninaziagiza wizara zinazohusika na usimamizi wa bodi hizi kuhakikisha bodi zinawezeshwa ili zitekeleze majukumu yake kwa ufasaha na kwa lengo lililokusudiwa,” amesema.

Awali Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Henry Mkunda amesema Shirikisho hilo linapendekeza kiwango cha kumwezesha mfanyakazi kuishi kiwe walau Sh milioni 1,010,000 kwa mwezi.

“TUCTA inatambua changamoto zilizotokana na UVIKO – 19 dunia pia vita ya Urusi na Ukraine vilivyopelekea kuyumba kwa uchumi duniani, lakini bado TUCTA tunaiomba serikali iweke kiwango halisi kitaifa cha malipo ya kima cha chini cha mishahara kitakachowezesha pamoja na wategemezi wao kuishi.

“Aidha, tunakumbuka pia ahadi yako ya kuboresha mishahara kwa wafanyakazi katika mwaka huu wa 2022, hivyo TUCTA tunapendekeza kiwango cha kumwezesha mfanyakazi kuishi kiwe walau Sh milioni 1,010,000 kwa mwezi baada ya hizi tafiti kufanyika. Kama itawezekana Mama tutashukuru sana kama utaliona hilo,” amesema.

error: Content is protected !!