RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa viongozi wanne. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Uteuzi huo, ameufanya leo Jumanne tarehe 30 Machi 2021, ukiwa ni uteuzi wa kwanza tangu alipoingia madarakani 19 Machi 2021, baada ya aliyekuwa Rais John Pombe Magufuli kufariki dunia 17 Machi 2021.
Baada ya kifo hicho, Samia aliyekuwa makamu wa Rais, aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania.
Taarifa iliyotolewa na Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu imeeleza, uteuzi wa viongozi hao, umeanza jana Jumatatu tarehe 29 Machi 2021.
Walioteuliwa ni; Dk. Florencs Turuka kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma.
Dk. Turuka anachukua nafasi ya Dk. Charles Msonde ambaye amemaliza muda wake.
Pili, Rais Samia amemteua Mhandisi Richard Masika kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (Tanzania Engineering and Manufacturing Design Organization – TEMDO).
Dk. Masika anachukua nafasi ya Profesa Patrick Makungu ambaye muda wake umekwisha.
Tatu, Rais Samia amemteua Dk. Blandina Robert Lugendo kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (Fisheries Education and Training Agency – FETA).
Nne, Rais Samia amemteua Paulina Mbena Nkwama kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (Teacher’s Service Commission).
Kabla ya uteuzi huo, Nkwama alikuwa Katibu Tawala Msaidizi (Elimu) Mkoa wa Kilimanjaro na anachukua nafasi ya Winfrida Rutaindurwa ambaye amemaliza muda wake.
Leave a comment