October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia ateua RC, Jaji kesi ya kina Mbowe

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali akiwemo Jaji Mustapha Siyani kuwa Jaji Kiongozi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Uteuzi huo umetangazwa leo Ijumaa, tarehe 8 Oktoba 2021 na Jaffar Haniu, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu ya Tanzania.

Jaji Siyani anachukua nafasi iliyoachwa wazo na Eliezer Feleshi ambaye aliteuliwa hivi karibuni kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Kabla ya uteuzi huo, Siyani alikuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma.

Aidha, Jaji Siyani ndiye anayesikiliza kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya ugaidi inayomkabili, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Jaji Siyani alianza kusikiliza kesi hiyo baada ya Mbowe kumtaka Jaji Elinaza Luvanda aliyekuwa akiisikiliza kujitoa kwani walihisi hatowatendea haki naye akakubali akajitoa.

Ameteuliwa kipindi ambacho kesi ndogo ndani ya kesi kubwa ilikuwa imefungwa ushahidi na uamuzi wake umepangwa kutolewa tarehe 19 Oktoba 2021, Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujimu Uchumi, iliyopo Mawasiliano jijini Dar es Salaam.

Taarifa hiyo ya uteuzi, imeeleza Rais Samia amemteua Omar Othuman Makungu kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Kabla ya uteuzi huo, Makungu alikuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar.

Pia, Rais Samia amemteua Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Sophia Mjema kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Mjema anachukua nafasi ya Dk. Philemon Sengati ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Wateule wote hao, wataapishwa Jumatatu, tarehe 11 Oktoba 2021, Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma.

error: Content is protected !!