RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, leo Ijumaa tarehe 13 Agosti, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Rais na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Elsewedy Electric kutoka nchini Misri, Mhandisi Ahmed El Sewedy, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Katika mazungumzo hayo, Mhandisi El Sewedy amemfahamisha, Rais Samia kuwa kampuni yake mbali na kuwa miongoni mwa kampuni zinazojenga mradi wa kuzalisha umeme katika Bwala la Mwalimu Nyerere.
Pia, imewekeza katika miradi mingine na kutarajia kuwekeza zaidi hapa nchini.
Mhandisi El Sewedy amesema kampuni yake inajenga mitambo ya kuzalisha umeme wa megawati 2115 katika Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Aidha, amesema katika eneo la Kigamboni, Dar es Salaam, kampuni yake imejenga kiwanda cha kuzalisha nyaya za umeme, transfoma, vifaa vya kuzuia nyaya za umeme zisilete hitilafu na mita za umeme, ambacho kinatarajiwa kufunguliwa rasmi Desemba mwaka 2021.
Amesema kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yanayoendelea kuwekwa na Serikali, wameamua kuunga mkono na kuwekeza zaidi kwa kujenga eneo la viwanda lenye ukubwa wa mita za mraba milioni mbili ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha mbolea.
Mhandisi El Sewedy ameongeza anatarajia kuwekeza katika ujenzi wa reli ya kisasa, na katika kipindi cha miaka 2 atahamasisha makampuni takriban hamsini (50) kutoka Misri kuja kuwekeza hapa nchini.
Kwa upande wake, Rais Samia amemshukuru Mhandisi El Sewedy na kumuhakikishia kuwa Serikali itampa ushirikiano katika kutekeleza miradi hiyo ya maendeleo kwa muda muafaka.
Rais Samia amesema ujenzi wa eneo maalum la viwanda litasaidia kuchangia kwa kiasi kikubwa utoaji wa ajira na ujuzi.
Aidha, Rais Samia amemjulisha Mhandisi huyo kuwa kwa sasa Tanzania inapitia sheria na sera zake mbalimbali ili kujenga mazingira mazuri zaidi ya biashara na uwekezaji.
Taarifa ya mazungumzo hayo, imetolewa na Jaffar Haniu, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
Leave a comment