May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia ateta na Dangote, atoa maagizo

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amemuagiza Waziri wa Uwekezaji, Geoffrey Mwambe na Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo, watatue changamoto zinazokikabili Kiwanda cha Saruji cha Dangote, mkoani Mtwara. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Gerson Msigwa, Rais Samia ametoa agizo hilo leo Jumatatu tarehe 24 Mei 2021, baada ya kufanya mazungumzo na mmiliki wa kiwanda hicho, Alhaji Aliko Dangote, katika Ikulu ya Dar es Salaam.

“Rais Samia amemuagiza Mwambe, Prof. Mkumbo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Masauni, ambao wamehudhuria mazungumzo hayo, kufanyia kazi changamoto zote zinazokikabili kiwanda cha Dangote ili kiendelee kuzalisha kwa ajili ya kuleta manufaa yaliyokusudiwa,” imesema taarifa ya Msigwa.

Aidha, Rais Samia amempongeza Alhaji Dangote kwa uwekezaji alioufanya nchini na kumhakikishia kwamba, Serikali yake italinda uwekezaji wake kwa manufaa ya pande zote mbili.

Kwa upande wake, Alhaji Dangote amemuahidi Rais Samia kwamba, kampuni yake iliyowekeza nchini kiasi cha Dola za Marekani 770 Milioni (Sh. 1.761 Trilioni), itaendelea kuwekeza katika maeneo mengine ikiwemo mpango wake wa kujenga kiwanda cha kuzalisha mbolea.

“Tutaendelea kuwekeza Tanzania ili kuzalisha ajira, mapato ya nchi na kuinua ustawi wa wananchi wa Tanzania, nadhani anahitaji kuungwa mkono katika hili na tumemuahidi kuwa tutaendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa hapa Tanzania ili kuunga mkono anachokifanya, sisi tutazalisha ajira,” amesema Alhaji Dangote.

error: Content is protected !!