October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia ateta na bosi EU, ataka kujua mambo 4

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amekutana na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya (EU), Charles Michel ambaye ametaka maoni kutoka kwa mkuu huyo wa nchi kuhusu masuala manne. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mambo hayo; ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vya korona (UVIKO 19), Mabadiliko ya Tabia Nchi, hali ya usalama nchini Msumbiji na mapinduzi ya kidijitali.

Wawili hao wamekutana jana Jumatano, tarehe 22 Septemba 2021 nchini Marekani ambako wanashiriki Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) ambapo leo Alhamisi, Rais Samia atahutubia mkutano huo.

Michel alitaka kupata maoni yake kuhusu mambo hayo ambayo ni kipaumbele kwa Umoja wa Ulaya (EU), kwenye mahusiano yake na Afrika na utayari wa Umoja wa Ulaya kushirikiana na Tanzania kwenye maeneo hayo.

Rais Samia ameushukuru Umoja wa Ulaya kwa ushirikiano wake na kuelezea hatua ambazo Tanzania inachukua katika kukabiliana na UVIKO 19, hasa ikizingatiwa ugonjwa huo umeathiri sekta nyingi ikiwemo sekta ya utalii.

Pamoja na mambo mengine, Rais Samia ameeleza hatua mbalimbali ambazo Serikali inachukua katika kusambaza miundombinu ya afya.

Amesema bado kuna changamoto katika upatikanaji wa vifaa tiba na rasilimali watu na hivyo kuukaribisha Umoja wa Ulaya kuangalia namna ya kushirikiana na Tanzania katika maeneo hayo.

Kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi, Rais Samia amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoathirika na Mabadiliko ya Tabia Nchi na inalipa kipaumbele suala hilo katika kukabiliana nalo.

Pia, Rais Samia amehudhuria Mkutano wa kuadhimisha miaka 20 ya Tamko la Durban kuhusu kupinga ubaguzi wa rangi na aina zote za unyanyasaji.

Taarifa ya mazungumzo hayo imetolewa na Jaffar Haniu, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

error: Content is protected !!