RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametangaza kutengua uteuzi wa wakurugenzi wanne wa halmashauri (DED) ya Buchosha (Mwanza), Iringa, Mbeya na Singida Mjini baada ya kubainika kutumia vibaya fedha za UVIKO-19. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).
Ametangaza uamuzi huo leo Ijumaa, tarehe 4 Februari 2022 akizungumza na wananchi wa Magu mkoani Mwanza akiwa njiani kwenda mkoani Mara katika ziara ya siku nne.
Rais Samia amesema, wakati anatangaza mgawanyo wa Sh.1.3 trilioni mkopo kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) kugharamikia miradi mbalimbali ya maenfeleo, “nilisema kama mkurugenzi anataka kuona rangi yangu halisi achezee hizo fedha.”
Amesema wakurugenzi hao alitengua uteuzi wake anasubiri ripoti nyingine ya mkurugenzi wa Geita kutoka kwa timu yake pamoja na ile ya Waziri wa Tamisemi, Innocent Bashungwa.
“Wakurugenzi wa Buchosa, Iringa, Mbeya na Singida Mjini, nimewatengua sasa hivi na nasubiri ripoti yenu ila nimewatengua kabla ya ripoti yenu kwani mmekuwa na tabia ya kuwafichia fichia na yule wa Geita endeleeni na uchunguzi na mimi timu yangu inaendelea ikiniletea taarifa naye nitamtengua,” amesema Rais Samia
Mkuu huyo wa nchi amewaeleza wananchi kwamba, Serikali anayoingoza “imeapa kuleta maendeleo kwa wananchi hivyo wawaombee ili waweze kutekeleza hilo kwa ufanisi ili Tanzania iweze kustawi na kunawili.”
“Ndugu zangu kuna maneno yalizunguka zunguka kwamba hakuna elimu bure ni waongo, tumejenga vituo vya afya, walisema miradi mikubwa itasimama haijengwi imesimama, reli yetu ya SGR inajengwa na kufika 2025 roti tano zote zitakuwa zimejengwa,” amesema
Kuhusu Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, “bado linaendelea na ujenzi unafikia asilimia sitini na na ujenzi unaendelea na hatudaiwi. Tunawaomba wananchi wa Magu msidanganywe na sisi tutafanya kama walivyofanya watangulizi wetu.”
Leave a comment