October 21, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia atangaza neema watumiaji wa mafuta Tanzania

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameagiza kupunguzwa tozo zinazotozwa na taasisi mbalimbali katika bidhaa za mafuta nchini humo zenye thamani ya Sh.102 bilioni kwa mwaka. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Lengo la kupunguza bei za mafuta ni kuwapa unafuu wananchi. Miongoni mwa mafuta hayo ni ya taa, dizeli, petrol na ya kula.

Maagizo hayo ameyatoa leo Jumanne, tarehe 5 Oktoba 2021, wakati akipokea taarifa kutoka kwa Waziri wa Nishati, January Makamba kuhusu utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa kwa wizara hiyo kupitia mwenendo wa biashara ya mafuta na bei zake hapa nchini.

Utekelezaji wa maagizo hayo umeenda sambamba na marekebisho ya Kanuni mbalimbali zinazohusiana na tozo na yatachapishwa katika Gazeti la Serikali leo Jumanne.

Rais Samia amechukua hatua hii ili kukabiliana na upandaji wa bei za mafuta katika soko la dunia ambapo kwa muda mrefu imekuwa ikipanda kwa kiwango kikubwa na kuathiri watumiaji wa bidhaa hiyo hapa nchini.

Rais Samia Suluhu Hassan

Taasisi zinazoguswa na maelekezo ya kupunguzwa kwa tozo hizo ni Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (tozo ya udhibiti), Mamlaka ya Bandari Tanzania (tozo ya miundombinu), Mamala ya Mapato Tanzania (tozo ya kuchakata taarifa) na Shirika la Viwango Tanzania ( tozo ya kupima ubora wa mafuta kwenye meli na gharama ya uwekaji wa vinasaba kwenye mafuta).

Pia zimo, Wakala wa Vipimo Tanzania (tozo ya uhakiki wa ujazo wa mafuta melini), Wakala wa Usimamizi wa Meli (tozo ya forodha) na Mamlaka ya Serikali za Mitaa (ushuru wa huduma kwenye Halmashauri nne zenye maghala ya kupokea mafuta kwa jumla).

Halmashauri hizo ni Kigamboni na Temeke za Jijini Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.

Aidha, Rais Samia ameagiza ufanyike mchakato wa haraka wa kupeleka marekebisho ya Sheria Bungeni endapo zipo sheria nyingine zinazohitaji marekebisho ya haraka katika kukabiliana na kupanda kwa bei za mafuta hapa nchini, ili kumlinda mtanzania na gharama za maisha zinazotokana na kupanda kwa bei ya mafuta.

Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri Makamba, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, Ummy Mwalimu.

Wengine waliohudhuria ni, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Eliezer Feleshi, Katibu Mkuu Wizara ya Niashati, Mhandisi Leonard Masanja, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali na watendaji wa Taasisi mbalimbali.

Taarifa ya kikoa hicho, imetolewa na Jaffar Haniu, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

error: Content is protected !!