RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema, Serikali anayoingoza itautizama kwa umakini mwaka 2022 ili kutatua changamoto zinazowakabili wananchi. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Amesema hayo katika hotuba yake ya kuufunga mwaka 2021 na kuukaribisha mwaka 2022, aliyoitoa leo usiku Ijumaa tarehe 31 Desemba 2021.
Rais Samia amesema, baada ya kuelezea kwa uchache changamoto na mafanikio yetu kwa mwaka 2021, sasa nizungumzie kwa kifupi masuala mtambuka wakati tukiuelekea Mwaka 2022.
“Serikali inautizama mwaka 2022 kuwa ni mwaka wa kukabiliana na changamoto zinazopunguza uwezo wa wananchi katika kukabiliana na maisha ya kila siku,” amesema Rais Samia
Amesema, kama ilivyotamkwa kwenye Mpango wa Tatu wa Serikali wa Miaka Mitano wa 2021/2026, kwamba lengo kuu ni kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Rais Samia amesema, mwaka 2022 ni mwaka wa Sensa ya Watu na Makazi, “hivyo naendelea kuwahimiza Watanzania kujitokeza kuhesabiwa ili tuweze kupata Takwimu zitakazotusaidia katika kupanga kwa usahihi masuala yetu ya maendeleo.”
Aidha, kwa watumishi wote wa umma na sekta binafsi, nitoe rai kuwa ni vyema tukauanza mwaka mpya wa 2022 na lengo la kuongeza ufanisi katika uzalishaji na ubora katika utoaji wa huduma.
“Tuazimie kuinua uchumi na kustawisha hali zetu, na tuendelee kulipa kodi stahiki kwa ajili ya maendeleo ya nchi,” amesema
Leave a comment