December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia ataka wanawake kujitokeza kuhesabiwa, kushiriki uchaguzi CCM

Rais Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wanawake wote nchini kujitokeza kwa wingi katika zoezi la sensa linalotarajiwa kufanyika mwaka 2022 pamoja na Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na jumuiya zake kwa kuwa kugombea nafasi mbalimbali ni haki yao kikatiba. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo tarehe 20 Novemba, 2021 wakati akihutubia mkutano wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) uliofanyika katika Uwanja wa Maisara Visiwani Zanzibar. 

Katika mkutano huo ulioandaliwa na UWT kwa lengo la kumpongeza, umehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Rais wa Zanzibar, Dk. Husein Ali Mwinyi, marais wastaafu wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Amani Abeid Karume na viongozi wengine.

Mbali na kuwashukuru viongozi hao kwa kumuandaa kisiasa, pia amewashukuru wanawake kwa kumuunga mkono kwani kitendo hicho kimempa faraja na kumtia hamasa na ari ya kutumikia Taifa na uenyekiti wa CCM.

Amesema mwaka 2022 Taifa linakabiliwa na zoezi la sensa lenye madhumuni ya kuhesabu na kujua idadi yetu Watanzania kwamba wanawake na wanaume wako wangapi.

“Kawaida tunasema wanawake ni jeshi kubwa lakini hii ni kwa takwimu za sensa ya mwaka 2012, sasa ya mwakani inakuja kukataa au kuthibitisha lakini kwa hali inavyoonesha bado wanawake tutakuwa jeshi kubwa.

“Niombe tushiriki wote kike kwa kiume tukubali kuhesabiwa ili tupate idadi kamili ya watanzania na tuweze kujipanga kwa idadi halisi ya watu tuliyo nayo,” amesema.

Amesema iwapo Mtanzania akikimbia kuhesabiwa atakimbiza fungu lake kwa serikali na kufaidika na mafungu yanayopangwa kwa wengine hivyo kuwadhulumu waliokubali kuhesabiwa.

Pia ametoa wito kwa wanawake kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa CCM na jumuiya zake.

“Naomba wanawake wenzangu kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa mwakani wa chama na jumuiya zake katika kugombea nafasi mbalimbali.

“Niwasihi tusirudi nyuma kwani kugombea ni haki yetu. Naomba mjitokeze, wanawake walio katika nafasi za ndani ya chama na serikali walianzia nyadhifa za chini,” amesema. 

Aidha, amewataka wanaCCM kujiepusha na matendo yanayokiukia katiba, sheria, kanuni, taratibu za chama  hicho.

Pamoja na mambo mengine amesema uungwaji mkono na dua anazoombewa zimemfanya kupata faraja na kutiwa moyo katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Ninajua ukitaka kuona ndugu zako wanakusaidia subiri ufikwe na janga, nami kwa sababu nimefikwa na janga hili la kupewa kiti kikubwa cha kuongoza nchi hii… ndugu zangu wote mmesimama na kunishika mkono,” amesema.

Aidha, kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT, Gaudencia Kabaka amesema aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Amesema kuanzia Machi hadi Oktoba mwaka huu, jumla ya wanawake wajasiriamali 2511 wamepatiwa Sh bilioni 9.5 kama mkopo nafuu kupitia dirisha la wanawake la benki ambayo uliagiza ianzishwe ambayo ni Tanzania Commercial Bank.

Pia amemuahidi Rais Samia kusimamia uanzishwaji wa mabaraza ya kuwawezesha wanawake kiuchumi nchi nzima.

“Nafikiri sisi UWT tulitetereka, hatukukuelewa maana ya mabaraza haya, tulifikiri unataka kutunyang’anya UWT, lakini Rais nikuahidi leo katika hadhara hii kama ulivyotuagiza huko nyuma na umeendelea kurudia mabaraza haya tunayafufua nchi nzima tukisaidiana na Tamisemi.

“Tunaanzia na mkoa wa Pwani, tumeongea tumekubaliana nitazindua baraza la kwanza mkoa wa Pwani mwezi ujao,” amesema Kabaka.

error: Content is protected !!