November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia ataka wahitimu vijana Chuo cha Taifa cha Ulinzi

Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan ameuagiza uongozi wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kuangalia uwezekano wa kuchukua wanafunzi wenye umri mdogo zaidi ili watakapohitimu wawe na muda mrefu wa kufanya kazi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo tarehe 14 Novemba, 2021 wakati akizindua na kukabidhi jengo la Chuo cha Taifa cha Ulinzi Kunduchi jijini Dar es Salaam.

Amesema ameshuhudia wahitimu ambao baada ya mwaka au miaka mwili wanakwenda kustaafu huku shahada waliyoipata hawaitumii katika sehemu za kazi kwa muda mrefu.

Aidha, ameeleza kufurahishwa na mpango wa mafunzo mafupi hasa kwa watendaji wa serikali za mitaa, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, hii program imenifurahisha sana.

“Program hii sasa ndio iliyonipa hamasa nichemshe bongo bilioni nane za majengo ya washiriki nakwenda kuzitoa wapi. Lakini ahadi yangu kwenu nitakwenda kuzitafuta,” amesema Rais Samia.

Amesema kupata majengo ni hatua moja kwenye kuboresha elimu katika sekta ya ulinzi na usalama wa nchi, ila mitaala itakayofundishwa na mbinu za utoaji mafunzo ni lazima ziendane na wakati na kukidhi mahitaji ya fani husika.

“Kwa upande wa jengo sina wasiwasi nimeona jengo na vyumba mkakati, shukrani wakuu wa chuo wameweka mpaka chuo cha Amiri Jeshi mkuu.

“Majengo ni jambo moja, mazingira mazuri yameweka, lakini kujituma kwa walimu, mitaala na mbinu za kufundishia ndio jambo lingine na hizo ndizo sifa za vyuo vingi mashuhuri na NDC ni chuo kimoja mashuhuri katika ukanda wetu huu Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

“Hivyo ni imani mtatumia majengo haya kujiimarisha na hata ikiwezekana kutanua wigo wa masomo mnayotoa. Mmefanya vizuri kwenye mafunzo ya ngazi za Masters degree na kozi nyingine, muda umefika sasa kutanua wigo na nitafurahi siku moja mkinialika kuja kushuhudia mahafali ya wanaohitimu katika ngazi ya PDH,” amesema.

Amesema Chuo hicho ni muhimu katika kuwaandaa kuwanoa maofisa na watendaji wa serikali zote mbili na nchi jirani katika nafasi mbalimbali za uongozi.

“Kupitia chuo hiki serikali imepata watendaji wazuri wenye uweledi na uthubutu wa kufanya maamuzi yenye kuzingatia masilahi mapana ya Taifa kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiusalama na hatimaye kupiga hatua katika kujiletea maendeleo,” amesema.

Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi, Meja Jenerali Ibrahim Mhona

Awali Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo amesema chuo hicho kitakuwa na uwezo wa kupokea washiriki wengi kutoka nje ya nchi.

Amesema kukamilika kwake kutaongeza uwezo wa wahitimu kufanya maamuzi mbalimbali ya kimkakati, kisiasa, kusalama, kijamii, kiulinzi.

“Niwashukuru Serikali ya watu wa China kwa ufadhili wa mradi huu na miradi mbalimbali mikubwa hapa nchini,” amesema.

Aidha, amesema chuo kinaendelea kuwa na jengo la utawala na mafunzo pasipokuwa na makazi ya washiriki.

“Gharama ya kujenga jengo hilo tayari imewasilishwa kwenye bodi ya chuo ambayo ni Sh bilioni 7.8, tunaomba serikali yako ituwezeshe kidogokidogo,” amesema.

Awali Mkuu wa Chuo hicho, Meja Jenerali Ibrahim Mhona amesema wanatarajia kuendesha kozi fupi ya muda wa siku tano mwezi Februari 2022 ya kundi la 12 kwa wakuu wa wilaya, makatibu tawala wa wilaya, na watendaji wakuu wa wilaya.

“Kozi hiyo imelenga kuwapa mikakati namna ya kupanga kutekeleza, kusimamia maelekezo na maagizo yanayotoka ngazi za juu ili kuleta mafanikio yenye tija kwa taifa pasipokuathiri usalama wa taifa,” amesema.

error: Content is protected !!