January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia atajwa kesi ya kina Mbowe

Spread the love

 

MRAKIBU wa Polisi, Jumanne Malangahe, ameulizwa na upande wa utetezi katika kesi ugaidi nayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, kama kikosi kilichoshughulika katika kesi hiyo kilimfahamisha Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, safari za mwanasiasa huyo nje ya nchi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Malangahe aliulizwa swali hilo leo Jumanne, tarehe 11 Januari 2022 na Wakili wa utetezi, Peter Kibatala, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Mahojiano ya Wakili Kibatala na Malangahe yalikuwa kama ifuatavyo;

Kibatala: Unafahamu Mbowe ambaye kwa mujibu wa ushahidi wenu ni mastermind wa huu ugaidi, alisafiri kwenda nje ya Tanzania mara kadhaa?

Shahidi: Hilo sifahamu

Kibatala: Katika kikosi kazi chenu, wewe ulikuwa second comander wa top leader ACP Ramadhan Kingai, unafahamu kuna mtu aliyewahi kumuarifu Rais Samia kuhusiana na movement za kutoka Tanzania, kwenda nje ya Tanzania za Mbowe?

Shahidi: Hilo mimi silifahamu

Kibatala: Unafahamu alipopata taarifa hizo Rais Samia, kwamba Mbowe alitoroka Tanzania akakimbilia nje kukwepa tuhuma au upelelezi wa tuhuma za kigaidi?

Shahidi: Sifahamu

Kibatala: Katika ushahidi wenu umezungumzia kikosi kazi chochote kinachoshughulikia suala hilo, kwamba Rais Samia alipata taarifa huko ulizungumzia hicho kikosi kazi?

Shahidi: Sifahamu

Kibatala: Kwa ufahamu wako hizo taarifa ya kwamba, Mbowe alitoroka kukimbia upelelezi, hizo taarifa ni za kweli?

Shahidi: Hilo silijui, sikulifanyia kazi

Kibatala: Rais Samia aliitangazia dunia kuna watu walifungwa, iambie mahakama kuna mtu aliyewahi kufungwa katika suala hilo?

Shahidi: Hilo silijui, siwezi kuliongelea

Kibatala: Boss wako ACP Ramadhan Kingai akiwa chini ya kiapo mahakamani, anadai anafahamu Mbowe alitoka nje ya nchi na ali-organize surveillance (ufuatiliaji), Mbowe akiwa nje ya nchi?

Shahidi: Suala la inteljensia ni la mtu binafsi

Kibatala: ACP Kingai aliieleza mahakama ali-coordinet surveillance ya Mbowe akiwa nje ya nchi, wewe kama Second Comand unafahamu Mbowe alikuwa surveillance nje ya Tanzania?

Shahidi: Sifahamu

Kibatala: Kwa ufahamu wako wewe, iliwahi kuwekwa travel ban (zuio la kusafiri) kwa Mbowe, mtuhumiwa wa kumastermind tuhuma za ugaidi ku-escape nje ya mipaka ya Tanzania, ku-escape justice?

Shahidi: Hilo mimi silifahamu

Kibatala: Unafahamu hata nchi Mbowe alizitembelea kipindi cha 4 Agosti 2020, mpaka anakamatwa 21 Julai 2021?

Shahidi: Sifahamu nchi hizo

Kibatala: Which means hauna ufahamu wowote kuhusu mawasiliano yoyote kati ya mamlaka ya upelelezi ya Tanzaia na nchi ambazo Mbowe alisafiri, unafahamu?

Shahidi: Sikuwa kwenye upelelezi

Kibatala: Ugaidi unashughulikiwa nchi nzima, unafahamu mamlaka za uchunguzi za Tanzania, zilizowasiliana na mamlaka chunguzi za nchi ambazo Mbowe alitembelea?

Shahidi: Hilo mimi silifahamu

Kibatala: Ni kawaida kwa mamlaka za nchi hizi za kiupelelezi na uchunguzi, kuzuia utokaji nje wa mtuhumiwa ili kuzuia asitoroke, ni suala la kawaida?

Shahidi: Inategema

Kibatala: Kwa nini?

Shahidi: Kwa nini wanazuia au wanaruhusu

Kibatala: Mtu anyepanga tuhuma za ugaidi ni flight risk (hatari kaa usafiri wa anga) au sio flight risk?

Shahidi: Hilo siwezi kujibu

Kibatala alimuuliza maswali hayo SP Malangahe, kufuatia kauli ya Rais Samia, aliyoitoa katika mahojiano yake na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC Swahili), mwanzoni mwa Agosti 2021, ambapo alisema kwa kipindi kirefu Mbowe hakuwepo nchini, alikuwepo Nairobi nchini Kenya.

Rais Samia alisema, Mbowe alikamatwa na kuunganiishwa na washtakiwa wenzake katika kesi hiyo, baada ya Jeshi la Polisi kukamilisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni, waliokuwa makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Malangahe amemaliza kutoa ushahidi wake mahakamani hapo, kesi hiyo imeahirishwa hadi Alhamisi, tarehe 13 Januari 2022 ambapo Jamhuri wataendelea kuleta mashahidi.

error: Content is protected !!