Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Samia asema hataki siasa za fujo, awapa masharti wapinzani
Habari za Siasa

Rais Samia asema hataki siasa za fujo, awapa masharti wapinzani

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan
Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewataka wanasiasa nchini humo kufanya siasa za maendeleo, badala ya kufanya siasa za fujo na vurugu. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Rais Samia ametoa wito huo katika mahojiano yake na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), yaliyorushwa hewani leo Jumatatu, tarehe 9 Agosti 2021.

Kiongozi huyo wa Tanzania, amesema baada ya nchi kumaliza uchaguzi, inabidi wananchi waungane kulijenga Taifa, kwani fujo za kisiasa hazipendezi.

“Kitu ambacho hakipendezi, ni ile kutaka uhuru wa kufanya fujo za kisiasa.

Labda  mmemaliza uchaguzi Serikali imeundwa,  kinachotakiwa kuendelea ni kujenga nchi uwe una  chama gani,  wote mnakuja pamoja mnajenga nchi yenu ndicho kinachotakiwa kuwa,”

“Lakini kinapotokea chama wao wanataka kuitisha tu maandamano kila siku yasiyo mwisho,  labda leo mkutano huko, fujo vurugu ile hapana,” amesema Rais Samia.

Kuhusu madai ya misingi ya demokrasia kuvurugwa, Rais Samia amesema Tanzania ina demokrasia, bali vyama vya siasa havitumii majukwaa yaliyowekwa kisheria kwa ajili ya kutatua changamoto zake.

“Demokrasia ya kisiasa iko na hapa naomba nitofautishe,  baina ya demokrasia ya kisasa na fujo za kisiasa.  Demokrasia ya kisiasa ni nini? Demokrasia ya kisiasa tuna vyama vya siasa wana vyombo vyao,  wanajadili mambo yao,  mfano baraza la vyama vya siasa huko wanajichagua wenyewe wanajaidli mambo ya siasa wanaelewana huko,” amesema Rais Samia.

Akizungumzia zuio la mikutano vya vyama vya siasa, Rais Samia amesema mikutano ya ndani iliyoainishwa katika katiba za vyama hivyo, haijazuiwa kufanyika, isipokuwa wahusika wanapaswa kufuata sheria.

“Vyama vya siasa vimeundwa na katiba zao na kwenda kufanya kazi kwao kunategemea katiba zao, kwa mfano    chama changu cha CCM,  katiba yangu  inaniambia labda katika mwaka nitakuwa na vikao viwili vya NEC,  labda vikao sita vya Kamati Kuu na vingine vya  ngazi za chini. Hivyo vikao vimeelezewa wajumbe ni nani na hivyo vikao vinaendeshwa bila bughudha bila kuomba ruhusa Polisi,” amesema Rais Samia.

Alipoulizwa kwa nini amekawia kutimiza ahadi yake ya kufanya mazungumzo na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani, Rais Samia amesema atakutana nao, lakini kwa sharti la kuwa pamoja.

“Nimesema nitakutana nao,  lakini sikutaka kukutana nao wakiwa wamechambuka chambuka,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema,  Serikali yake itaendelea kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari na wa watu kujieleza.

“Wakati mwingine kusema kwao,  bora umpe mtu nafasi aongee alichonacho,  atoe umsikie. Kama kiongozi useme  kinalalamikiwa hiki, basi unakifanyia kazi kuliko ukiwabana hawasemi. Hujui wanafukuta na nini ndani,  sasa Tanzania kuna uhuru wa kutosha vyombo vyote vya habari viko huru,” amesema Rais Samia na kuongeza:

“Toka umefika umesikia vyombo vya habari vinalalamika?  Hakuna chombo kimelalamika,  kuna uhuru wa kutosha wa kujieleza na wanaojieleza mpaka wanavuka mipaka saa nyingine.  Lakini kwa sababu kiongozi inabidi mvae ngozi ngumu muangalie.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

error: Content is protected !!