May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia asamehe wafungwa 5,001

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa msamaha kwa wafungwa 5,001 waliokuwa wakikabiliwa na adhabu ya vifungo mbalimbali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Msamaha huo, unakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 57 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambao ulifanyika tarehe 26 Aprili 1964.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu, tarehe 26 Aprili 2021 na Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, imesema, miongoni mwa wafungwa hao, 1,516 wameachiwa huru baada ya kupunguziwa robo ya adhabu zao badala ya punguzo la kawaida la theluthi moja linalotolewa chini ya kifungu cha Sheria ya Magereza sura ya 58.

Amesema, wafungwa 3,485 wamepunguziwa robo ya adhabu zao badala ya punguzo la kawaida la theluthi moja linalotolewa chini ya kifungu cha 49 (1) cha Sheria ya Magereza sura ya 58.

Msigwa amesema, wafungwa 3,485 waliopunguziwa adhabu zao wataendelea kutumikia sehemu ya kifungo iliyobaki.

Rais Samia amewataka wafungwa wote walioachiwa huru, kutumia vyema mafunzo waliyoyapata wakiwa gerezani na waungane na wananchi wenzao katika ujenzi wa Taifa huku wakiheshimu na kuzingatia sheria.

Aidha, Rais Samia, amewatakia heri Watanzania wote katika maadhimisho ya miaka 57 ya Muungano na amewataka kutumia siku hii kutafakari juhudi mbalimbali zilizofanyika katika ujenzi wa Taifa na wajibu wa kila mmoja katika kuendelea kujenga Taifa imara.

Ameahidi kuendelea kuuenzi, kuulinda na kuundeleza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa manufaa ya Watanzania wa pande zote mbili.

error: Content is protected !!