RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema tuzo ya Babacar Ndiaye ya 2022, inayotolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), kwa ajili ya kutambua nchi iliyofanya vizuri katika ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji, alipaswa kupewa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Mkuu huyo wa Tanzania, ametoa kauli hiyo leo Jumatano, tarehe 25 Mei 2022, jijini Accra nchini Ghana, baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo kwa niaba ya Serikali yake ya Awamu ya Sita.
“Nikitambua napokea tuzo hii nikiwa bado siamini kwamba tuzo hii inaweza kuwa ya mtu binafsi, mimi naamini tuzo hii inatakiwa iwe ya mtu mmoja lakini anayestahili kuliko wote Tanzania ni Dk. John Magufuli,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema, jitihada za ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji zilianzishwa katika awamu tano za uongozi zilizopita, lakini katika jitihada hizo Hayati Magufuli ajitokeza zaidi kwa kuwa alikuwa Waziri wa Ujenzi katika Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Hayati Benjamin Mkapa na Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Jakaya Kikwete.
Akizungumzia maendeleo ya Bara la Afrika, Rais Samia amewashauri wakuu wa nchi kuweka mikakati madhubuti ya usimamizi wa rasilimali za bara hilo ikiwa pamoja na kuimarisha ukanda wa biashara, ili zinufaishe wananchi.
Ili kufanikisha hilo, Rais Samia ameshauri nchi za Afrika kuimarisha miundombinu ya usafirishaji hasa barabara na reli, kwani ni kigezo muhimu katika kuunganisha bara hilo na fursa za kiuchumi.
Duh!
Mama umesema kweli.
Je, utaikabidhi kwa familia ya Hayati Magufuli iwekwe kwenye makumbusho yake?