June 21, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia apangua wakuu wa mikoa, Chalamila atoswa

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, leo Ijumaa tarehe 11 Juni 2021, amefanya mabadiliko madogo ya wakuu wa mikoa ya Mara, Mwanza na Tabora. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa ya mabadiliko hayo imetolewa mapema leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Jaffar Haniu.

Taarifa ya Haniu imesema, Rais Samia amemhamisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhandisi Robert Luhumbi, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, akichukua nafasi ya Albert Chalamila, ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

“Mkuu wa Mkoa wa Mara, Luhumbi, anahamia mkoa wa Mwanza, ambapo aliyekuwa mkuu wa mkoa, Chalamila, uteuzi wake umetenguliwa,” imesema taarifa ya Haniu.

Albert Chalamila, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza

Kwa mujibu wa taarifa ya Haniu, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ally Hapi, amehamishiwa mkoani Mara, huku Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Batilda Buriani, akiteuliwa kurithi mikoba ya Hapi mkoani Tabora.

“Aidha, Zuwena Jiri ambaye ni Katibu Tawala Wilaya ya Simanjiro, ameteuliwa kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, kuchukua nafasi ya Batilda,” imesema taarifa ya Haniu.

Taarifa hiyo imesema, tarehe ya uapisho wa viongozi wapya, itatangazwa baadae.

Mabadiliko hayo yanafanywa ikiwa ni wiki kadhaa, tangu Rais Samia afanye mabadiliko na uteuzi wa wakuu wa mikoa nchi nzima, baada ya kuingia madarakani tarehe 19 Machi 2021, kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi

Magufuli alifariki akiwa madarakani, tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu ya ugonjwa wa moyo.

Mwili wake ulizikwa nyumbani kwao Chato mkoani Geita, tarehe 26 Machi mwaka huu.

Tarehe 15 Mei 2021, Rais Samia alifanya mabadiliko ya wakuu wa mikoa, ambapo Chalamila aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, alimhamishia Mwanza.

error: Content is protected !!