January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia aonya wawekezaji kuzungushwa

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo kwa wasaidizi wake, kutowabudhudhi wawekezaji hususan wazawa kwani kufanya hivyo kunachelewesha fursa za ajira. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Aidha, amewataka kuanzia sasa, kuanza kuuelezea kwa lugha nyepesi na inayoelewekwa kwa wananchi mpango wa ‘Blue Print.’

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Ijumaa, tarehe 3 Desemba 2021, wakati akizindua kiwanda cha kutengeneza nyaya za mawasiliano cha Raddy Fiber, kinachomilikiwa na Mtanzania, Ramadhan Hassan Mlazi, kilichopo Mkuranga, mkoani Pwani.

Mwekezaji huyo alianza kufuatilia suala la uwekezaji mwaka 2015, katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), wakati mkurugenzi wake akiwa Godfrey Mwambe ambaye kwa sasa ni Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu- Uwekezaji.

Amesema, ametembelea kiwanda hicho na kushuhudia vijana wa Kitanzania wakiwa wameajiriwa jambo linalotoa moyo licha ya mwekezaji huyo kukumbana na changamoto alipotaka kuwekeza.

“Mwekezaji huyu, ameanza kuwepo nchini kuwekeza mwaka 2015, leo ni 2021, ni miaka sita, ni hakika amekumbana na misukosuko, changamoto, ucheleweshaji wa kiwanda. Aliyemchelewesha (Godfrey Mwambe,) leo amekuja kufungua,” amesema Rais Samia

“Sasa Waziri Mwambe, yasimamie yanayochelewesha uwekezaji, yarekebishwe ili wawekezaji wapite haraka hara,” amesema

Rais Samia amesema, mwekezaji huyo kwa sababu ni mzawa, alipokwenda kuelezea lengo lake “walimwona ni dalali, mwongo…waziri naomba muache hizo kasumba, kuna Watanzania wengi ambao sasa wamekwisha kutembea, wamepata mitaji, wamejikusanya, naomba mjiwekeze.”

Kiongozi huyo wa nchi, amempa pole mwekezaji, Mlanzi “nakupa pole kwa milima na mabonde uliyokumbana nazo.”

Amesema, Serikali anayoingoza, inahakikisha inaweka mazingira rafiki ya uwekezaji hivyo asingependa kuona wasaidizi wake wanamwangusha.

“Tumeweka wazi nchi yetu tunawahitaji zaidi wawekezaji kuliko wao wanavyotuhitaji. Hatuna budi kufanya kila linalowezekana, kuwachuja na kuangalia anayefaa. Unapomchelewesha mwekezaji, unachelewesha ajira. Hawa wawekezaji wamekopa benki, unapomchelewesha, unamchelewesha kurejesha mikopo yao,” amesema

Aidha, ametumia fursa hiyo, kutoa wito kwa wasaidizi wake, kuuelezea mpango wa Blue Print kwa wananchi, ili uweze kueleweka vizuri.

“Hili jambo la Blue Print limekuwa likisemwa muda mrefu na hawa wasaidizi wangu na mawaziri, kila wakisimama wanasema Blue Print, nikawauliza halina Kiswahili chake, nawagiza semeni kiswahili watu waelewe na muutafasiri kwa lugha rahisi kabisa,”

Amegusia kwa ufupi, Blue Print ni mpango ulioweka mapendekezo ya kurahisisha uwekezaji ndani ya nchi, kuweka kodi zinazofaa, kurahisisha miundombinu yote na kurahisisha njia ya kuwekeza na kufanya biashara.

error: Content is protected !!