RAIS Samia Suluhu Hassan, ameonya Watanzania wanaotumia mitandao ya kijamii kuchonganisha watu. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Kiongozi huyo wa Tanzania ametoa onyo hilo leo Alhamisi tarehe 22 Aprili 2021, akihutubia Bunge jijini Dodoma.
Rais Samia amesema hayo wakati akikemea taarifa za uzushi juu ya chanzo cha kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk. John Magufuli, kilichotokea tarehe 17 Machi 2021, kwenye Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam.
“Nikemee vikali wale walioko kwenye mitandao, ndugu zangu dini zetu zinasema na ni kanuni ya maisha, tunakuja duniani na tunaondoka duniani.
nimekuwa nikiona kwenye mitandao na nadhani wanaofanya hivyo wanajua kwamba hatutaweza kuwapata, wanatumia mifumo huko mingine ambayo bado hatujawa na uwezo wa kuwatafuta lakini niwamabie tutawatafuta,” amesema Rais Samia.
Mrithi huyo wa Dk. Magufuli amewataka watu hao kama wanaushahidi wa kutosha wauwasilishe katika vyombo vya uchunguzi kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
“Nimekuwa nikiona kwenye mitandao taarifa za uchonganishi, taarifa tuliyopewa na madaktari wetu ya kifo cha Dk. Magufuli ni kutokana na tatizo la udhaifu wa moyo ambalo ameishi nalo kwa muda wa miaka 10.
Kuna watu wamejitokeza kwenye mitandao huko fulani na fulani wamempa sumu, fulani na fulani walikuwa wametega kitu hiki. Sasa niwaambie kama wanataraifa za maana waje tuwasikilize, vyombo vya upelelezi na uchunguzi vipo waje tuwasilikize,” amesema Rais Samia.
Leave a comment