August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia aomba utulivu miji iliyokosa miradi ya maji

Spread the love

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameitaka miji iliyoachwa katika miradi ya maji ya miji 28, kuwa na utulivu kwa kuwa Serikali yake inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuifikisha kwenye maeneo yake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Rais Samia ametoa wito huo leo Jumatatu, tarehe 6 Juni 2022, katika hafla ya utiaji saini mikataba ya miradi ya maji ya miji 28, iliyofanyika Ikulu, jijini Dodoma.

Kiongozi huyo ameitaja miji iliyokosa miradi hiyo, ikiwemo ya Same na Mwanga, ambapo changamoto hiyo ilisababishwa na changamoto za kisheria. Huku akiahidi Serikali yake inatafuta fedha kiasi cha Sh. 36 bilioni, kwa ajili ya kufikisha maji katika maeneo hayo.

“Wakati leo tunazungumza maji hapa, kuna miji ambayo inajiuliza mbona hatujatajwa na miji inayojiuliza sana ni miji ya Same na pale Mwanga. Sababu nazungumza na Watanzania wote niwatie moyo ndugu zangu tulikuwa na tatizo la kisheria kwenye miji hii. Tumeshafanyia kazi tunakwenda kutatua tatizo la upatikanaji maji,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema “tutakwenda kupekuwa wapi tunaweza kuzipata fedha (Sh. 36 bilioni), katika miradi mirefu ya siku nyingi inatekelezwa na kusimama ni Same na Mwanga, tutakwenda kutafuta fedha tuhakikishe mwakani wenzao wakipata fedha na wao wapate fedha.”

Aidha, Rais Samia ametaja miji mingine iliyoachwa katika miradi hiyo, kuwa ni Mji wa Dodoma, ambapo amesema Serikali yake ina mpango wa kujenga bwawa la Farkwa, pamoja na kuanzisha mradi wa kusambaza maji kutoka Bwawa la Mtera.

Kuhusu miradi ya maji katika miji 28, Rais Samia amewaagiza watendaji wa wizara ya maji hususan wahandisi, kuwasimamia wakandarasi wanaoitekeleza, ili ikamilike kwa ufanisi.

“Nawahakikishia wananchi kuwa miradi hii itanufaisha miji yote 28, hakuna mji utaachwa,. Niwaase kuwa mzidi kuendelea kutekeleza na kutimiza vipaumbele vyenu kama livyoeleza,” amesema Rais Samia.

Maeneo yatakayonufaika na miradi hiyo yenye thamani ya zaidi ya Sh. 1 trilioni, ni Wilaya ya Muheza, Handeni, Pangani mkoani Tanga. Miji ya Makambamo, Wang’ing’ombe, Mafinga, Ludewa, Makambako, Nanyumbu, Mpanda, Sikonge, Kaliua, Manyoni, Chemba, Chamwino na Chato.

error: Content is protected !!