Spread the love

IMEELEZWA kuwa kukamilika kwa ujenzi wa Kituo cha Afya Kifunda kilichopo Kata ya Lupilo katika Halmashauri ya Busokelo mkoani Mbeya, kumeokoa jahazi la wanakijiji wa Kifunda baada ya kukwama kukamilisha ujenzi wa kituo hicho tangu mwaka 2017. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Wakizungumza na MwanaHalisi Online hivi karibuni wamesema ujenzi wa Kituo cha Afya Kifunda ulianza kwa nguvu za wananchi na wadau wa maendeleo kwa kuchangia michango mbalimbali lakini ilisuasua tangu mwaka 2017.

Akizungumzia athari walizokuwa wakizipata kutokana na ukosefu wa huduma za afya kijijini hapo, Brown Mwambilu alianza kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada alizofanya kuhakikisha ujenzi huo unaendelea.

“Tulikuwa tunapata athari kubwa kwa kukosa huduma ya afya, ukiangalia hapa tulipo ili upate huduma za afya inabidi utembee kwa zaidi ya kilomita 48.

“Kutoka hapa kwenda Kituo cha Afya Itete bado ni kilomita zaidi ya 10, kwa hiyo ni athari katika kupata huduma ya afya,” amesema.

Kauli hiyo ya iliungwa mkono pia na mkazi mwingine wa kijiji hicho, Huruma Kamara ambaye amesema kituo hicho cha afya kitakapokamilika kitawasaidia wananchi wengi hususani akina mama na watoto.

“Itatupunguzia adha ya sisi akina mama kujifungulia njiani na kupunguza vifo vya akina mama wanaojifungua na watoto wachanga,” amesema.

Naye Tuitike Ikono amemshukuru Rais Samia na kuongeza kuwa akina mama ndio wanaopata changamoto zaidi pindi huduma za afya zinapokuwa mbali.

“Namshukuru Rais ametuona wanawake shida tulizokuwa tunazipata,” amesema.

Aidha, Mganga Mkuu Halmashauri ya Busokelo, Christopher Mwasongela amesema uwepo wa kituo hicho utawasaidia wananchi kutotembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.

“Huku ni milima na mabonde, mvua inanyesha kila mara na usafiri wenyewe bado ni tabu kwa sababu barabara zetu bado hazijakaa vizuri.

“Kwa hiyo kwa kupatikana kwa kituo hiki kunawapunguzia adha ya kusaka huduma mbali katika kituo cha afya,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *