RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amemwalika Rais wa Marekani, Joseph Biden kutembelea nchini humo ili kuzidi kuimarisha uhusino uliopo kati ya nchi hizo mbili. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Ametoa mwaliko huo, jana Jumanne, tarehe 06 Julai, 2021, alipofanya mazungumzo kwa simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken.
Blinken amempongeza, Rais Samia kwa kushika hatamu ya uongozi nchini na kumhakikishia kuwa Serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuleta maendeleo kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kwa kuzingatia vipaumbele vya nchi.

Katika mazungumzo hayo, Blinken amepongeza Rais Samia kwa hatua anazozichukua kukabiliana na ugonjwa wa Corona nchini Tanzania na Marekani ipo tayari kuisaidia Tanzania katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Aidha, Blinken amepongeza jitihada za Rais Samia katika kuimarisha Demokrasia nchini ikiwa ni pamoja na azma yake ya kukutana na kushirikiana na vyama vya siasa pamoja na kusimamia Uhuru wa vyombo vya habari.
Pia, amepongeza uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara na kuahidi kuwa hali hiyo imeivutia Marekani kushawishi wawekazaji wake kuja kuwekeza nchini.
Kwa upande wake, Rais Samia ameshukuru kwa pongezi na kuahidi kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Marekani kukuza uhusiano baina ya nchi hizi mbili katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa.
Rais wetu kuzungumza na waziri wa mambo ya nje wa Marekani? Protokali ya wapi? Kwanini Biden asizungumze na Mama? Tusijidhalilishe