October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia amwaga mabilioni Geita

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa Sh.28.6 bilioni kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Geita. Anaripoti Mwandishi Wetu, Geita … (endelea).

Majaliwa amesema Rais Samia anataka kuona kila Mtanzania anapata huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za afya, elimu, maji, nishati ya umeme na miundombinu katika makazi yao.

Aliyasema hayo jana Jumanne, tarehe 12 Oktoba 2021, wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Muganza katika wilaya ya Chato mkoani Geita.

Alisema kati ya fedha hizo shilingi bilioni 16 zimepelekwa wilayani Chato.

Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa mkoa wa Geita kuhakikisha fedha hizo ambazo zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji, elimu, barabara na afya zinatumika kama ilivyokusudiwa.

Akizungumzia kuhusu changamoto ya upungufu wa watumishi wa sekta ya afya, Majaliwa alisema Serikali inaendelea kuajiri ili kuhakikisha lengo lake la kufikisha huduma bora za afya kwa wananchi linafikiwa.

Kadhalika, Majaliwa aliuagiza uongozi Wakala wa Majin a Usafi wa mazingira Vijijini (Ruwasa) wilaya ya Chato uhakikishe kiasi cha Sh. 5.2 bilioni kilichotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji zinatumika vizuri na wananchi wapate huduma hiyo.

Majaliwa aliwaagiza viongozi hao wahakikishe wanaanza kufanya utafiti ili waweze kutumia maji ya Ziwa Victoria kwa kuyasambaza kwa wananchi. Alisema haiwezekani watu wanakaa karibu na ziwa na hawana maji ya kutosha.

Awali, Mbunge wa Chato (CCM), Dk. Medrad Kalemani alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika wilaya hiyo kama ujenzi wa barabara, miradi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu, vituo vya afya pamoja na miradi ya maji.

error: Content is protected !!