Rais Samia Suluhu Hassan leo Ijumaa amemvua hadhi ya Ubalozi Dk. Wilbroad Slaa kuanzia tarehe 01 Septemba, 2023.
Dk. Slaa aliteuliwa kuwa Balozi tarehe 23 Novemba 2017 na Rais awamu ya Tano hayati, Dk. John Magufuli. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu imethibitisha madai ya Dk. Slaa kuwa tangu aanze kupinga mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi kati ta Serikali ya Tanzania na Dubai, amekuwa akipokea vitisho vya kuvuliwa hadhi ya ubalozi.
Dk. Slaa ambaye amekuwa kinara wa kupinga mkataba huo ambao pia Dubai kupitia kampuni ya DP World itawekeza kwenye bandari za Tanzania, tayari alikamatwa pamoja na wenzie kutokana na tuhuma mbalimbali za uhaini kisha kuachiwa kwa dhamana.
Tarehe 12 Julai mwaka huu, Mbunge huyo wa zamani wa Karatu na Katibu mkuu mstaafu wa Chadema, alisema baada ya kupiga kelele kuhusu mkataba huo amepigiwa simu na kutishiwa na watu kutoka serikalini kwamba akae kimya na akiendelea kupiga kelele watamvua hadhi ya ubalozi mara moja!
“Najua maneno hayo ni makali… nimepokea vitisho na mimi pia sio kwa mawakili tu, wengine wakasema ubalozi wako tutachukua, nawaambia chukueni sasa hivi…siishi kwa ajili ya ubalozi. Nimesema sina chama najiamini najau ninachosimamia.
“Nitasema siku zote, CCM au Chadema ikifanya mema nitapongeza, anayeharibu yeyote nitamsema bila kumung’unya maneno, bila kuona aibu na kwa hili hakuna aibu tutakwenda wote,” alisema Dk. Slaa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Leave a comment