RAIS Samia Suluhu Hassan amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko, ili kupisha uchunguzi wa ubadhirifu wa fedha Sh. 3.9 Bilioni, uliofanyika katika mamlaka hiyo.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).
Kiongozi huyo mpya wa Tanzania amechukua hatua hiyo leo Jumapili tarehe 28 Machi 2021, baada ya kupokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020.
CAG Kichere ameikabidhi ripoti hiyo kwa Rais Samia, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
“Imani yangu ni kwamba, kama kuna ubadhirifu ndani ya shirika na kwa ripoti ile uliyonipa jioni, kuna uibadhirifu Sh. 3.9 Bil. karibu Sh. 4 Bil.
Waziri Mkuu(Kassim Majaliwa) alivyofanya ukaguzi walisimamishwa wa chini, naomba nitoe agizo la kumsimamisha mkurugenzi mkuu wa bandari halafu uchunguzi uendelee,” ameagiza Rais Samia.
Rais Samia amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Brigedia Jenerali, John Mbungo, kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo.
“Katika ripoti yako nimeona pia ubadhirifu mkubwa umefanywa katika shirika la bandari TAKUKURU hii ni kazi maalumu jishughulishe pale,” ameagiza Rais Samia.
Awali CAG kichere alisema katika ukaguzi wake, amebaini ubadhirifu TPA, na kueleza kwamba, ofisi yake inaendelea na ukaguzi wa ubadhirifu huo.
“Ukaguzi tuliofanya katika mashirika mbalimbali ya Serikali, tumegundua changamoto kadhaa ambazo zinahitaji serikali kukagua, ikiwemo matatizo katika Shirika la Bandari, ubadhirifu ambao tunaendelea kufanya ukaguzi katika maeneo hayo,” amesema CAG Kichere
Leave a comment