December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia ampa maagizo mazito IGP, askari kukimbilia trafki, bandarani kizungumkuti

Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro kufuatilia na kumpa majibu kuhusu sababu za askari wengi wanaohitimu mafunzo kung’ang’ania wapangiwe katika kitengo cha askari wa usalama barabarani ‘trafki’ au bandarini. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)

Pia amemuagiza kutumia vifaa vya kisasa kufanya ukaguzi wa magari ili kuuza stika nyingi na kupata mapato yatakayoliwezesha Baraza la la Taifa la Usalama Barabani kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Anaripoti Mwandishi Wetu… (endelea)

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo tarehe 23 Novemba, 2021 wakati akihutubia katika maadhimisho ya Wiki nenda kwa usalama barabara yaliyofanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Maadhimisho hayo yalienda sambamba na kauli mbiu ya ‘Jali maisha yako na ya wengine barabarani.’

Akizungumzia suala la askari wengi kuomba kujiunga na trafki au bandari baada ya kuhitimu mafunzo yao, alitolea mfano kijijini kwake kwamba aliwahi kupokea maombi ya vijana wawili kwa nyakati tofauti wakimuomba awasaidie wajiunge na vitengo hivyo.

“Nikamuuliza wa kwanza kwanini unaomba lazima upangwe trafki? akanijibu kwamba ‘ukipangwa huko unanyanyuka harakara haraka, maisha yanakunyookea.

“Lakini wa pili akanijibu kule kwetu kuna trafki anaitwa cheupe huwa anaongoza misafara ya viongozi kwa mbwembwe kwelikweli akiwa njiani, kwa hiyo aliniambia anamhusudu sana cheupe, kwa upande mmoja cheupe amewa-  inspire vijana wajiunge lakini huyu mwingine anasema nikikosa trafki nipangwe bandarini, sasa IGP hebu rekebisha hilo,” amesema.

Aidha, amesema kwa kuwa kundi kubwa la vijana ndio wahanga wakubwa wa ajali za barabarani, ni vema Jeshi la Polisi kutumia simu za viganjani kutoa elimu ya usalama barabara badala ya redio na running pekee.

“Kwa sababu vijana wengi wapo kwenye mitandao hiyo, pengine hawana muda wa kusikiliza au kutazama lakini mkiwaendea kwa simu zao za viganja mtafikia vijana wengi zaidi,” amesema.

Amemuagiza IGP Sirro kuweka msukumo mkubwa kwenye eneo la utafiti kuhusu masuala ya usalama barabarani ili kupata suluhu ya kisayansi na kimfumo ya namna ya kupunguza ajali za barabara.

“Shirikianeni ya vyuo vikuu vya usafirishaji na ufundi vilivyopo nchini, mnaweza kukaa na kujadili kwa upana, mkafanya utafiti na kuona jinsi ya kupunguza ajali hizo,” amesema.

Amesema katika kutekeleza jukumu la kusimamia la usalama barabara askari wanatakiwa kuwa msaada kwa wananchi na sio kero.

“Wananchi wakiwaona wawakimbilie sio wawakimbie, kwa sababu ajali nyingine zinatokana na hawa vijana wa pikipiki akiona uniform ziko pale anakata kichochoro huko mbele hajui kuna nini ajali zinatokea.

“Kwa hiyo askari mjitahidi kuwa wenyewe wa usalama barabarani, muwe rafiki na mnaofanya nao kazi, muwe kimbilio la watu wanaotumia barabara,” amesema.

Pia amesema kuna kero ndogondogo kama za  kushikilia leseni za madereva kwa muda mrefu au kulazimisha madereva kulipa faini papohapo wakati sheria inampa muda dereva kulipa faini.

“Kuna ukamataji mkubwa wa vyombo vya moto, ukipita katika vituo vya polisi utakuta pikipiki nyingi zimepangwa, nyingine hazionekani kama zimekatwa jana na leo.

“Utajiuliza kwanini haziondoki pale kwa sababu kama ni ushahidi wa makosa, makosa yasikilizwe, kesi zimalizike ahukumiwe mkosaji, kazi iendelee, lakini vyombo vinabaki muda mrefu, pengine unahisi vimetelekezwa na wenyewe, nadhani iangaliwe kwa undani kero hizi zinasababishwa na nini,” amesisitiza.

Aidha, amewakata wadau wa usalama barabarani washirikiane katika suala la usalama barabarani na mapambano dhidi ya ajali za barabarani badala ya kuendekeza malalamiko.

“Kwa sababu nilipopita kwenye mabanda kule nimekuta malalamiko kibao, Taboa wanasema lao, Latra wanasema lao, kaeni kitako muelewane, ni mazungumzo pekee yatafanya mambo yaende vizuri ikibidi kubadilisha sheria, kanuni tubadilishe. Wote tunajenga nyumba moja,” amesema.

error: Content is protected !!