December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia amaliza ziara Arusha, arejea Dodoma

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amehitimisha ziara yake ya siku tano katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha na kurejea Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma leo Jumatatu, tarehe 18 Oktoba 2021. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).

Alitua Uwanja wa Ndege wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), tarehe 14 Oktoba 2021, akitokea Chato mkoani Geita, katika kilele cha Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru na Kumbukizi ya kifo cha Hayati, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kesho yake yaani tarehe 15 Oktoba 2021, alizundua barabara ya Sanya Juu-Elerai yenye kilomita 32.2, wilayani Siha na kuzungumza na wananchi wa eneo hilo. Kisha siku hiyohiyo, aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa wodi ya mama na mtoyo katika Hospitali ya mkoa ya Mawenzi-Moshi.

Baadaye, alikwenda kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la Rau na kuwasalimia wananchi waliojitokeza kwenye uzinduzi huo.

Jioni ya siku hiyo, Rais Samia alihutubia mkutano mkubwa wa hadhara, katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.

Siku inayofuata, tarehe 16 Oktoba 2021, alikuwa mgeni rasmi katika maadhimosho ya Yubile ya miaka 50 ya Hospitali ya KCMC, Moshi, ambapo aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la mionzi katika hospitali hiyo na kuzindua manara wa kumbukizi ya miaka 50.

Mara baada ya kumaliza Kilimanjaro, Rais Samia alikwenda mkoani Arusha ambapo jana Jumapili tarehe 17 Oktoba 2021, alizindua mradi wa maji wa Chekereni uliopo Arumeru pamoja na kuzindua Hospitali ya Jiji la Arusha iliyopo eneo la Njiro Arumeru.

Baadaye, Rais Samia akahutubia mkutano mkubwa wa hadhara katika uwanja wa Amri Abeid jijini Arusha.

Siku ya mwisho ya zaiara yake leo Jumatatu, tarehe 18 Oktoba 2021, Rais Samia ameanza kwa kuzindua kiwanda cha nyama cha Eliya Food Overseas LTD kilichopo Eurendeke kisha kuzindua mradi mkubwa wa majisafi na salama eneo la stendi mpya, Longido ambapo alizungumza na wananchi wa eneo hilo.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, Rais Samia ameagana na viongozi mbalimbali wa chama cha mapinduzi na serikali wakiwemo wakuu wa mikoa ya Kilimanjaro, Stephen Kagaigai na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella.

Alipowasili Uwanja wa Ndege wa Dodoma, Rais Samia amepokewa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, akiwemo mkuu wa mkoa huo, Anthony Mtaka.

error: Content is protected !!