May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia akwamisha kongamano la TCD

Rais Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kimesogeza mbele kongamano la haki, amani na maridhiano, hadi tarehe 4 na 5 Aprili 2022, sababu zikitajwa aliyepangwa kuwa mgeni rasmi, Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa na majukumu mengine. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TCD, Bernadetha Kafuko, kupitia ukurasa wa Twitter wa kituo hicho, siku sita kabla ya kongamano hilo kufanyika jijini Dodoma, ambalo lilipangwa tarehe 30 hadi 31, Machi mwaka huu.

Taarifa ya Kafuko imesema, ratiba ya kongamano hilo imeingiliana na vikao vya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho Mwenyekiti wake ni Rais Samia.

CCM kinatarajia kufanya vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu (NEC), tarehe 31 Machi 2022, wakati Mkutano wake Mkuu Maalumu kwa ajili ya kufanya marekebisho ya katiba, ukipangwa kufanyika tarehe 1 Aprili mwaka huu, jijini Dodoma.

“Napenda kuchukua fursa hii kuwataarifu kuwa, kutokana na ombi rasmi la Rais Samia, ambaye ratiba yake imeingiliana na vikao vya chama chake, mkutano wetu wa kitaifa wa haki, amani na maridhiano, umesogezwa mbele hadi tarehe 4 na 5 Aprili, 2022,” imesema taarifa ya Kafuko.

Aidha, taarifa ya Kafuko imesema, ajenda na ratiba za kongamano hilo zitaendelea kama zilivyopangwa awali.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya TCD, tayari taarifa hiyo imesambazwa kwenye vyama wanachama wa kituo hicho, ikiwemo ACT-Wazalendo, Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi.

Aidha, Kamati ya Ufundi ya TCD, imemuelekeza Kafuko kuzungumza na Chadema, juu ya msimamo wake wa kutoshiriki kongamano hilo, kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa hoja zao.

“Mkurugenzi mtendaji ameleekezwa na kikao cha kamati ya ufundi, aendele kuwasiliana na Chadema, kuona ushiriki wao kwa sababu wao bado ni wanachama. Kwa hiyo taarifa zote wanapelekewa,” amesema afisa wa TCD ambaye hakutaka kutaja jina.

error: Content is protected !!