SAMIA Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania, amemteua Yusuf Tindi Mndolwa kuwa Balozi. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Arusha … (endelea).
Pia, Rais Samia amemteua Balozi mteule Mndolwa kuwa Mkuu wa Itifaki (Chief of Protocol) katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Taarifa iliyotolewa jana usiku Jumamosi, tarehe 17 Aprili 2021, na Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu imesema, Mndolwa anachukua nafasi iliyoachwa na Balozi Wilbert Ibuge ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Msigwa amesema, Balozi mteule Mndolwa, ataapishwa kesho Jumatatu tarehe 19 Aprili, 2021 Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Wakati huo huo, Rais Samia amemteua, Benedict Ndomba kuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).
Kabla ya uteuzi huo, Ndomba alikuwa Mkurugenzi wa Miundombinu na Operesheni wa eGA na anachukua nafasi ya Dk. Jabir Bakari Kuwe ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Uteuzi wa viongozi hao umeanza jana Jumamosi tarehe 17 Aprili, 2021.
Leave a comment