May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia aanza kupekua miradi ya JPM

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema amepitia mikataba ya miradi ya ujenzi wa miundombinu, iliyoachwa na mtangulizi wake, Hayati John Magufuli, aliyefariki dunia akiwa madarakani, tarehe 17 Machi 2021.Anaripoti Nasra Bakari, DMC…(endelea).

Kiongozi huyo wa Tanzania wa Awamu ya Sita, amesema hayo leo Jumanne, tarehe 1 Juni 2021, alipotembelea ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka ‘Mwendokasi’, kutoka Gerezani hadi Mbagala Kuu, mkoani Dar es Salaam.

Rais Samia amesema, alipokuwa anapitia miradi hiyo, alibaini ujenzi wa mradi wa Mwendokasi Mbagala ulioanza mwezi Machi 2019, unasuasua.

“Ndugu zangu nilikuwa napitia mafaili ya miradi ofisini, nikauona mradi huu wa mwendokasi kuelekea Mbagala , kwa sasa hivi ulikuwa ufikie kama asilimia 60. Lakini kwa taarifa ambazo nimezikuta na kupata leo, mradi huu uko asilimia 16 tu,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema, Serikali yake imezungumza na mkandarasi anayejenga barabara hiyo, ili kuangalia kinachokwamisha ujenzi wake.

“Nikaona mimi na timu yangu tuangalie kitu gani kinakwaza mradi huu kuendelea, tumeongea na wakandarasi na wasimamizi wa mradi, tumeona kitu gani kinachelewesha mradi lakini kiujumla kama Serikali hatujaridhika na kasi ya mradi unavyoendeshwa, tumeona mwisho mwisho wameongeza spidi,” amesema Rais Samia.

Mradi huo unatekelezwa na kampuni za China ya Sino Hydro Cooperation, Kampuni ya Botek inayoshirikiana na APEX. Kampuni ya China Civil Engineering Construction Cooperation (CCECC) na Inter Consult, chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).

Rais Samia amesema Serikali yake imewaagiza wakandarasi hao wamalize ujenzi wa mradi huo haraka.

“Tumetaka wamalize mradi, tumejitathimini upande wa Serikali na mnasikia juzi tumebadilisha kiongozi wa mradi, tumemuweka mwingine ili atusaidie kuonegeza kasi ya utekelezaji mradi huu,” amesema Rais Samia.

Mradi wa Mwendokasi Mabagala, ni miongoni mwa miradi ya miundombinu iliyoachwa na Magufuli, aliyeiongoza Tanzania katika Serikali ya Awamu ya Tano, kwa miaka mitano na miezi mitano mfululizo (Novemba 2015-Machi 2021).

Magufuli alifariki dunia kwa ugonjwa wa moyo, katika Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam. Kisha mwili wake ulizikwa nyumbani kwao Chato mkoani Geita, tarehe 26 Machi 2021.

error: Content is protected !!