October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia aanika sababu kuigawa wizara ya afya

Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema anatarajia kuigawa Wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto na kuunda wizara ya maendeleo ya jamii ili kutoa msukumo katika utekelezaji wa mipango na sera za masuala ya usawa wa kijinsia. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea)

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo tarehe 16 Disemba, 2021 jijini Dodoma wakati akizindua kamati ya ushauri kitaifa ya utekelezaji wa ahadi za nchi kwenye jukwaa la kizazi chenye usawa.

Amesema amefarijika kuona kuwa wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya afya, ustawi wa jamii, jinsia, wazee na watoto – Zanzibar zinafanya kazi ya uratibu na jitihada zinaendelea kufanyika kuhakikisha kuwa yale yote waliyoahidi yanatekelezwa vema.

Amesema anaelewa kuwa wizara hizo mbili zimekuwa zikifanya kazi kwa karibu ikiwa ni pamoja na maandalizi ya tukio hilo.

“Sasa ndugu zangu unaweza kuona kwamba pamoja na jitihada zote tulizozifanya na sera zote tulizoweka lakini bado hatujafika tulipotakiwa kufika. Sasa ili tuweze kufika tunapotakiwa kufika, ni lazima kuwe na usimamizi, uratibu, utathmini na ufuatiliaji wa sera na utekelezaji wetu wa mipango

“Wizara hizi ukizitizama ni afya na-na- na…, maamuzi yangu ni kuitenga wizara itakayoshughulikia jinsia, wanawake na mambo mengine,” amesema huku akishangiliwa na wadau waliohudhuria uzinduzi huo.

Amesema wizara ya afya ikiwekwa na mambo mengine na hali iliyopo sasa duniani, sekta ya afya peke yake inachukua sura kubwa ya wizara hiyo kuliko vile vipengele vingine vilivyobaki.

“Lakini kama tutatenga vipengele vingine vilivyobaki na afya tukaisimamisha peke yake usimamizi wa sera, sheria na mambo mengine unaweza kwenda vizuri na ukapata msukumo unaohitaji.

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Dk. Dorothy Gwajima

“Kwa hiyo hayo ndio maamuzi na ninatajaribu kumshawishi Rais wa Zanzibar ili naye afanye vivyo hivyo ili tuende vizuri,” amesema.

Aidha aemsema baada ya miaka 20 tangu kutolewa kwa azimio la Beijing la kumkomboa mwanamke, bado serikali nyingi duniani zimeshindwa kutekeleza sera za kumuinua mwanamke kiuchumi.

Amesema kumekuwa na vikwazo vingi katika maeneo ya afya, elimu, mila kandamizi, upatikanaji wa mitaji, teknolojia inayoweza kuwarahisishia kazi zao, masoko, huduma za ugani, hifadhi ya jamii na unyanyasaji wa aina mbalimbali.

“Muda umefika sasa kufanyia kazi kikamilifu sera na sheria zinazotungwa na mipango tunayoweka kwa ajili ya kuinua hali ya uchumi ya kuleta ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla,” amesema.

error: Content is protected !!