May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia aagiza uchunguzi tukio mauaji Dar

Rais Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameliagiza Jeshi la Polisi nchini humo, lifanye uchunguzi wa kina kuhusu tukio la mauaji ya watu wanne na majeruhi sita, lililotokea maeneo ya Ubalozi wa Ufaransa, mkoani Dar es Salaam. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Amri Jeshi huyo mkuu ametoa agizo hilo leo Jumatano, tarehe 25 Agosti 2021, saa chache baada ya tukio hilo kutekelezwa na mtu mmoja aliyekuwa na silaha, kwenye makutano ya barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Kinondoni, mkoani humo.

Aidha, Rais Samia ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza ndugu zao katika tukio hilo.

“Natoa pole kwa Jeshi la Polisi na familia za Askari 3, na Askari 1 wa kampuni ya ulinzi ya SGA waliopoteza maisha baada ya mtu aliyekuwa na silaha kuwashambulia katika eneo la Salenda, Dar es Salaam,” amesema Rais Samia

“Mtu huyo amedhibitiwa na hali ni shwari. Nawaagiza Polisi kuchunguza kwa kina.”

Mtu huyo ambaye hadi sasa hajajulikana jina, alitekeleza mauaji hayo, kisha baadae alidhibitiwa na Jeshi la Polisi. Aliuawa wakati akijibizana kwa risasi na Askari Polisi.

Awali, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo ya Jeshi la Polisi, CP Liberatus Sabas, amesema jeshi hilo limeunda timu ya kuchunguza tukio hilo.

“Tumeshaanzisha timu ya upelelezi, muda si mrefu tutakamilisha uchunguzi. Kama mtu ana uhusiano na mtendaji wa tukio, upelelezi utatuambia huyu mtu wa namna gani,” amesema Kamanda Sabas.

Miongoni mwa watu waliofariki dunia ni Askari Polisi watatu na Askari wa Kampuni ya Ulinzi ya SGA.

Majeruhi wa tukio hilo wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam.

error: Content is protected !!